Sunday, November 19, 2017

Beki Manchester United amtesa Jose Mourinho

 

Jose Mourinho ameibua vita kali ya maneno baada ya kulaumu madaktari wa Chama cha Soka cha England (FA), akidai beki wake, Phil Jones alichomwa sindano sita kabla ya kuchezea timu ya taifa.

Jones alishindwa kuendelea na mchezo huo dhidi ya Ujerumani ulioisha kwa suluhu baada ya kupata maumivu ya misuli.

Mourinho amesema beki huyo wa kati alipigwa sindano sita za kutuliza maumivu ili acheze mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa.

Pia Mourinho amemshukia kocha wa England Gareth Southgate kwa kumtumia mchezaji akijua kuwa alikuwa majeruhi.

“Kumpiga mchezaji sindano sita za kutuliza maumivu katika mchezo wa kirafiki, sijapata kuona,” alisema Mourinho.

Alisema Southgate anatakiwa kuwahoji madaktari wa England kwa tukio hilo alilodai halikuwa la kawaida na ametaka uchunguzi zaidi ufanyike.

“Sikuwahi kuona mchezaji mmoja akichomwa sindano sita kwa wakati mmoja tena katika mchezo wa kirafiki,” aling’aka kocha huyo Mreno.

Ijumaa iliyopita, FA ilitoa taarifa kuwa imeshitushwa na kauli ya Mourinho, na kutetea uamuzi wa mchezaji huyo kuchomwa sindano sita kwa madai kwamba ni jambo la kawaida.

-->