Berlusconi kurejea tena katika soka Italia

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi ambaye kwa sasa anautajiri unaofikia zaidi ya dola 8 bilioni za kimarekani, ametimiza miaka 81, anamiliki kiasi kikubwa cha hisa katika kampuni ya Mediaset, aliimiliki klabu ya A.C. Milan kuanzia mwaka 1986 hadi 2017.
  • Aliuza hisa zake na kujiondoa katika umiliki wa klabu ya AC Milan, mwaka jana lakini sasa anapanga kurudi tena kwa kutaka kununua timu.

Milan, Italia. Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi, ambaye pia ni mdau mkubwa wa soka, amepanga kurudi tena baada ya kukaa nje ya soka kwa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa katika gazeti la Gazzetta dello Sport, mmiliki huyo wa zamani wa klabu ya AC Milan amepanga kuinunua timu ya daraja la tatu ‘Serie C’ ya Monza FC.

Berlusconi aliyepigwa marufuku kujihusisha tena na masuala ya kisiasa  amepanga kununua timu hiyo kupitia kampuni yake ya Fininvest ambayo ipo jijini Milan, ikiripotiwa kuwa amekubali kutoa kati ya Euro 2.5 milioni hadi tatu.

Bilionea huyo ameahidi kutumia uzoefu wake pamoja na kuwekeza fedha za kutosha kuhakikisha timu hiyo inapanda hadi kucheza Ligi Kuu Italia ‘Serie A’

Berlusconi, aliuza AC Milan kwa muwekezaji kutoka China kwa dola 800 milioni ingawa alichelewa kulipwa fedha hizo hadi kufikishana kwenye vyombo vya sharia lakini ameshazipata na inaonekana zimechangia kuongeza utajiri wake.

Mkataba wa kuinunua Monza na makabidhiano kamili yanatarajiwa kufanywa hivi karibuni na makamu Rais wa zamani wa AC Milan, Adriano Galliani na ndiye atakayekuwa mtendaji mkuu wa timu hiyo.