Biashara yaenda sambasamba na Simba, Yanga yasajili wa kimataifa

Muktasari:

  • Biashara imepanda kucheza ligi kuu msimu huu pamoja na timu nyingine za Alliance ya Mwanza, Coastal Union ya Tanga, JKT Tanzania, KMC na African Lyon za Dar es Salaam.

Mwanza. Klabu ya Biashara United ya Mara, imeingia anga za Simba na Yanga kwa kuwasajili wachezaji wanne kutoka Ivory Coast, Guinea, Nigeria na Burkinafaso.

Wachezaji hao ambao wamesajiliwa kwa kandarasi ya miaka miwili kila mmoja ni mlinda mlango, Balora Nourdine wa Burkinafaso, beki wa kati, Nkourouma Wilfried wa Guinea, washambuliaji Austine Amos raia wa Ivory Coast na Alex Francis wa Nigeria

Meneja wa timu hiyo, Aman Josiah amesema, usajili huo ni mwanzo wa maandalizi yao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na wamejiandaa kufanya vizuri na kuleta ushindani kwenye soka.

“Leo (Jumatano) tunawatambulisha wachezaji wetu wapya ambao wataitumikia timu yetu inayojiandaa na ligi hii kwa msimu ujao, tunaamini watatusaidia kufikia malengo yetu,”alisema Josiah.

Ameongeza kuwa, zoezi hilo la usajili litaendelea na wataongeza wachezaji wengine wasiopungua watano kutoka ndani ambao ni wazoefu na ligi kuu na tayari wameshaanza kufanya mazungumzo nao.

“Tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wachezaji lengo tuwapate wasiopungua watano ambao ni wazoefu na wanafanya vizuri ligi kuu,mkakati ukiwa ni kuandaa timu yenye ushindani,”alieleza Meneja huyo.