Boban awaibua Mayay, Tigana

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Yanga kumsajili kiungo mshambuliaji nguli, Haruna Moshi ‘Boban’ wadau wa michezo wameibuka kuhusu usajili wa nyota huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars.

Boban jana alitia saini mkataba wa miezi sita, akitokea African Lyon na usajili wake umeibua mjadala kwa wadau wa michezo kutokana na umri na mwenendo wa tabia yake uwanjani.

Baadhi ya wadau wana amini Boban hawezi kudumu Yanga muda mrefu kutokana na rekodi yake ya tabia uwanjani licha ya kutajwa kuwa ni mchezaji mwenye kipaji cha aina yake.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo raia wa Brazil aliwahi kutamka kuwa Boban ni mchezaji wa aina yake aliyewahi kumuona Tanzania.

Maximo alimtaja Boban ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kwa ufanisi.

Usajili wa Boban umemuibua mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay ambaye alisema mchezaji huyo siyo wa malengo ya muda mrefu, lakini ujio wake Yanga utaiongezea timu hiyo utulivu na ubunifu katika eneo la ushambuliaji.

“Hicho ndicho alichokuwa anawasaidia hata Lyon ingawa siyo usajili wa malengo ya muda mrefu, lakini kwa muda mfupi atawasaidia. Kuna watu wana wasiwasi na Boban katika nidhamu, lakini sidhani kama atawasumbua Yanga kwa sasa amekomaa,” alisema Mayay.

Naye kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Yusuph ‘Tigana’ alisema Boban ana kiwango cha kuitumikia timu yoyote kubwa nchini kwa sasa.

“Kiwango chake ni kikubwa, bado mwili wake unaonakana kutochoka sio mchezaji wa kumtegemea kwa mipango ya muda mrefu ila anaweza kuipa Yanga mafanikio.

“Uwezo wake huwezi kumlinganisha na mchezaji yeyote kwa sasa.Kama Yanga watawezana naye wanaweza kupata ubora wake mkubwa uwanjani,” alisema Tigana.

Yanga imemsajili wa mkongwe huyo kutokana na mapendekezo ya Kocha Mwinyi Zahera aliyevutiwa na kiwango cha mchezaji huyo katika mechi za Ligi Kuu msimu huu.