Bocco azua jambo Simba

Muktasari:

  • John Bocco ana rekodi ya kuifunga Yanga mabao 15 katika mashindano tofauti

Dar es Salaam, Shinyanga. Kukosekana kwa nahodha John Bocco katika mchezo dhidi ya Yanga ni pengo kubwa kwa Simba, licha ya uwepo wa kundi kubwa la washambuliaji nyota kwenye kikosi hicho msimu huu.

Bocco alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro, dakika ya 81 baada ya kumpiga ngumi kichwani Revocatus Richard wa Mwadui FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ambao Simba ilishinda mabao 3-1.

Kadi hiyo itamfanya Bocco akose mchezo unaofuata wa Simba ambayo itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ingawa anaweza kujikuta akiongezewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya 38 ya Ligi Kuu.

“Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga/kupigana atasimama kushiriki michezo mitatu (3) inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya Shilingi 500,000 (Laki tano),” inafafanua ibara ya tatu ya kanuni hiyo ya udhibiti kwa wachezaji.

Michezo mitatu ambayo Bocco ataikosa ni dhidi ya Yanga, African Lyon na Stand United.

Kukosekana kwa Bocco kwenye mechi dhidi ya Yanga huenda kukaigharimu zaidi Simba kuliko timu nyingine kutokana na uzito wa pambano hilo la watani wa jadi.

Benchi la ufundi la Simba bila shaka litaumiza kichwa katika kipindi cha wiki moja ya maandalizi kutafakari ni nani hasa ataweza kuziba vyema pengo la Bocco katika mechi dhidi ya Yanga ili kupata ushindi.

Kumkosa Bocco maana yake kunailazimisha Simba kumpanga Mganda Emmanuel Okwi kwenye nafasi aliyokuwa akicheza mwenzake jambo ambalo huenda likapunguza ufanisi wa safu ya ushambuliaji ya Simba.

Okwi aliyepumzimshwa katika mchezo wa juzi, atapangwa pacha na Meddie Kagere ambaye amekuwa chaguo la kwanza la Simba katika nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Pengo la Bocco linaweza kuonekana katika mchezo huo kwa kuwa Okwi ameonekana kutoendana na kasi na kushindwa kuelewana na Kagere kwa kuwa katika mechi mbili dhidi ya Ndanda na Mbao FC, Simba haikufurukuta.

Hata hivyo, kigezo hicho hakiondoi maana kuwa Okwi ni mshambuliaji tishio na amekuwa mwiba kwa Yanga na sio mchezaji wa kubeza katika mechi zinazokutanisha watani wa jadi.

Okwi anaweza kufanya maajabu kulingana na aina ya mfumo ambao atatumia Kocha Patrick Aussems, baada ya kumkosa Bocco katika safu ya ushambuliaji.

Pia kukosekana Bocco huenda kukawapunguzia presha mabeki wa Yanga katika kudhibiti mashambulizi kupitia mipira ya kona, krosi na adhabu ndogo, kutokana na uwezo wa nahodha huyo kuunganisha kwa vichwa mipira ya aina hiyo na kufumania nyavu.

Kingine ambacho Simba itakosa kwa Bocco kwenye mechi dhidi ya Yanga ni uzoefu wake mbele ya wapinzani wao tofauti na nyota wengine waliopo kwenye kikosi chao.

Rekodi nzuri ya mshambuliaji huyo kufumania mabao dhidi ya Yanga, kwa kiasi kikubwa ingeongeza presha na hofu kwa mabeki wa wapinzani wao tofauti na Okwi ambaye hana takwimu za kuvutia za kuifunga Yanga.

Bocco ameifunga Yanga mabao 15 katika mashindano tofauti ambayo amewahi kukutana nayo wakati Okwi amefunga manne tu dhidi ya timu hiyo tangu alipotua nchini.

Mbali na Okwi, Simba ina nafasi ya kumtumia mshambuliaji mmoja kati ya Adam Salamba au Mohammed Rashid kucheza nafasi ya Bocco ingawa wawili hao hawajapata nafasi ya kutosha kucheza tangu msimu ulipoanza.

Pia Aussems anaweza kulazimika kubadili mfumo na kucheza 4-2-3-1, kwa kumuanzisha Kagere kama mshambuliaji pekee wa kati, huku nyuma kukiwa na viungo washambuliaji watatu akina Shiza Kichuya, Cletus Chama, Hassani Dilunga au Mohammed Ibrahim.

Aussems alisema kuwa pengo la Bocco linatarajiwa kuzibwa na mchezaji ambaye amemuandaa kwa mchezo dhidi ya Yanga akidai kuwa ana uwezo wa kufanya vyema.