Wednesday, September 13, 2017

Bugando wazungumzia hali ya Mc Pilipili

 

By Jonathan Musa, Mwananchi

Hali ya mchekeshaji maarufu nchini, Emmanuel Mathias maarufu Mc Pilipili aliyepata ajali ya gari bado haijaimarika, imeelezwa.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikolazwa Mc Pilipili, Lucy Joseph amesema yupo katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu akisubiria kufanyiwa vipimo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amesema chanzo cha ajali ni mwendokasi.

Amesema ajali hiyo ilitokea jana Jumanne saa kumi jioni katika Barabara ya Mwanza – Shinyanga.

Haule amesema ndani ya gari aina ya Toyota Prado mali Mc Pilipili walikuwa watu watatu.

Kamanda Haule amesema dereva wa gari hilo alikuwa Saidi Hassan (28), mkazi wa Dar es Salaam na walikuwa wakitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam.

Gari hilo amesema liliacha njia na kupinduka na kwamba, Mc Pilipili amepata majeraha sehemu mbalimbali mwilini ikiwemo kifuani.

Kamanda Haule amesema dereva alipata michubuko mkono wa kulia.

Katibu Muhtasi wa Kampuni ya Pilipili Events, Stella Maswenga alisema jana kuwa walipokea taarifa za ajali hiyo jana Jumanne jioni.

Maswenga alisema Mc Pilipili alialikwa mkoani Shinyanga kwa ajili ya kusherehesha harusi wikiendi iliyopita.

-->