Burkina, Mkamba Rangers mdebwedo

Muktasari:

Burkina FC imepoteza michezo mitatu na kupata  sare moja wakati Mkamba Ranger ikitandikwa michezo miwili na kupata sare mbili ikiwa imebakia mchezo mmoja kufunga panzia la mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Burkina FC na Mkamba Rangers zote za Morogoro zimeendelea kugawa pointi katika ligi daraja la pili  inayoendelea kutimua vumbi.

Burkina FC imepoteza michezo mitatu na kupata  sare moja wakati Mkamba Ranger ikitandikwa michezo miwili na kupata sare mbili ikiwa imebakia mchezo mmoja kufunga panzia la mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Katika baina ya timu hizo mshambuliaji wa Burkina, Joseph Nditi aliipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya nne kabla ya Mkamba Rangers kusawazisha kupitia Stanlaus Mkachoe dakika ya 29 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Wakizungumza baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, makocha wa Burkina na Mkamba walitoa sababu za timu zao kufanya vibaya huku wakiahidi kufanya vizuri katika mzunguko wa pili.

Kocha wa Burkina FC, Damian Mussa alisema kudorora na kushindwa kupata ushindi kwa kikosi chake kumetokana na kukosa bahati licha ya juhudi za wachezaji uwanjani.

Damian alisema wamepoteza michezo mitatu na kuambulia sare moja kati ya michezo minne na matokeo hayo hajawakatisha tamaa kwani yametokana na kukosa bahati licha ya vijana wake kusakata kabumbu safi lakini wamekosa kutikisa nyavu na kujikuta wakikung’utwa na wapinzani wao.

“Tunajipanga na mchezo wa mwisho wa duru la kwanza ili tupate matokeo kwani utasaidia kuturudisha kwenye mbio za kuwania nafasi ya kwanza ligi daraja la kwanza na tumeweka mikakati ya kuanza mzunguko wa pili na nguvu mpya.”alisema Damian.

Kocha wa Mkamba Rangers, Nicolaus Makata alisema kushindwa kupata matokea mazuri katika michezo ya ligi hiyo kumetokana na mapungufu katika idara zote huku wakikosa wachezaji wazoefu, licha ya yeye kukabidhiwa timu ikiwa imepoteza michezo miwili.

Makata alisema kuwa wanajiandaa na mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya huku wakiwa na matumaini ya kuibuka kidedea ili kuwarejesha kwenye ushindi wa ligi hiyo.