Bwalya apewe ulinzi Simba

Dar es Salaam. Wakati Kocha Patrick Aussems wa Simba akitambia safu kali ya ushambuliaji inayoundwa na nyota watatu, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco, Nkana Red Devils inatambia mpachika mabao wake mahiri Walter Bwalya.

Bwalya ndiye habari ya mjini kwa upande wa Zambia, baada ya vyombo vya habari nchini humo kumtaja kuwa ndiye mchezaji atakayeibeba Nkana katika mchezo wa Jumamosi.

Simba na Nkana zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu hizo kufuzu mechi zao za hatua ya awali.

Wakati Simba ikimtegemea kiungo Clatous Chama kuwa sehemu kubwa ya kupata matokeo katika mchezo huo, Nkana inabebwa na Bwalya ambaye anatajwa ndiye mshambuliaji tishio katika Ligi Kuu Zambia.

Chama ndiye alikuwa mpishi mkuu wa matokeo mazuri iliyopata Simba katika mechi zote mbili dhidi ya Mbabane Swallows nyumbani na ugenini.

Vyombo vya habari nchini humo vimemtaja Bwalya ndiye mhimili wa timu kupata matokeo mazuri kutoka na uwezo wake mzuri wa kutumia mguu wa kushoto.

Mbali na kucheza eneo kubwa la ushambuliaji uwanjani, Bwalya ana sifa ya ziada ya kurudi nyuma kuomba mipira na kupasua ngome ya wapinzani na amekuwa akifanya hivyo katika mechi mbalimbali zikiwemo za kimataifa.

Nkana imekuwa ikimtumia Bwalya kufunga na kutengeneza mabao yao kutokana na kasi aliyonayo, akitumia zaidi mguu wa kushoto ‘kuficha’ mpira.

Nahodha huyo mwenye miaka 23, amepewa kijiti cha kuiongoza Nkana baada ya Idris Mbombo aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zambia msimu uliopita kujiunga na Al Hilal ya Sudan.

Mshambuliaji huyo alifunga mabao 10 huku mfungaji bora wa mashindano hayo msimu uliopita akiwa Mbombo aliyefunga 21.

Katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Barclays ambalo Nkana ilitwaa, Bwalya aliisumbua ngome ya Zesco United inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina.

Bwalya aliingia Nkana ikiwa nyuma kwa bao 1-0, kuchukua nafasi ya Ronald Kampamba, alichangia ushindi wa mabao 2-1 baada ya kutoa pasi zilizozaa mabao hayo yaliyofungwa na Mbombo.

Katika mchezo wa Jumamosi mtu pekee anayeweza kumdhibiti Bwalya ni kiungo mkabaji James Kotei ambaye ana uwezo mzuri wa kukaba kuanzia katikati.

Kotei ana fursa ya kumdhibiti Bwalya endapo atapewa jukumu na Aussems kwa kuwa atakuwa na nafasi nzuri ya kwenda naye kokote uwanjani kulinganisha na mabeki wa kati.

Kwa kuwa Kotei anacheza namba sita, ana nafasi ya kumdhibiti mshambuliaji huyo kulinganisha na Pascal Wawa na Erasto Nyoni wanaotarajiwa kucheza kama mabeki wa kati.

Katika kuonyesha Bwalya siyo mchezaji wa kawaida, kigogo cha soka Algeria, USM Algiers kilirusha ndoano ya kutaka saini yake Januari, mwaka huu. Hata hivyo, akiwa Algeria mpango uligonga mwamba baada ya viongozi wa pande zote mbili kushindwa kufikia mwafaka.

Mchezo wa Jumamosi utakuwa wa tano kwa miamba hiyo kwani mwaka 1994 Nkana ilishinda mabao 4-1 nchini Zambia kabla ya Simba kushinda 2-0 Dar es Salaam katika Kombe la Washindi Afrika. Nkana ilishinda jumla ya mabao 4-3.

Mwaka 2002 timu hizo kongwe katika soka zilikutana katika mchezo wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, Nkana ilishinda mabao 4-0 nchini Zambia na ziliporudiana Dar es Salaam, Simba ilishinda 3-0.