Yanga yaangukia Kombe la Shirikisho Afrika

Muktasari:

Yanga sasa wanasubiri ratiba ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika

Dar es Salaam. Baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, nahodha ya Yanga, Nadir Haroub amesema wanahitaji kujifunza kutumia vizuri mechi za nyumbani kama wanataka kufanya vizuri katika soka la kimataifa.

Yanga imetolewa na Township Rollers leo Jumamosi baada ya kutoka suluhu ugenini hivyo kuondolewa kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 waliopata Wabotswana hao katika mchezo wa kwanza.

Akizungumza baada ya kumaliza kwa mechi nchini Botswana, Nadir 'Canavaro' alisema  wanatakiwa kukomaa na kutumia nafasi katika michezo ya nyumbani  na kupata matokeo ili kuwa na kazi rahisi ugenini.

"Tumecheza vizuri katika vipindi vyote, lakini bahati mbaya tumetolewa na sasa tunaaangalia Kombe la Shirikisho Afrika'.

"Muhimu ni kuhakikisha tunajitahidi sana kupata matokeo mazuri katika michezo yetu ya nyumbani ili tukija ugenini kama hivi tunakuwa na kazi rahisi kwa sababu ugenini kuna mambo mengi"alisema  Canavaro.

Hata hivyo Yanga licha ya kutolewa katika mashindano hayo imeangukia katika mashindano Kombe la Shirikisho Afrika ambayo hatua ya mtoano itafanyika kati ya April 6 na 7.

Miamba mingine iliangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni St. George ya Ethiopia, Zanaco (Zambia), UD Songo (Msumbiji) michezo mingine inaendelea leo na kesho.

Katika mchezo huo Yanga ilianza vizuri, lakini kadri muda ulivyoendelea ilionekana kuzidiwa na wapinzani wao hivyo kuwafanya mabeki Kelvin Yondani na Andrew Vincent kuwa na kazi kubwa ya kuokoa hatari nyingi golini kwao.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara walifanya mashambulizi machache golini kwa wapinzani wao tofauti na Township Rollers ambao muda mwingi wa mchezo hasa kipindi chote cha pili walikuwa wakilisakama lango la Yanga kama nyuki.

Shambulizi la maana ambalo Yanga ilifanya katika kipindi cha kwanza ni dakika ya 39  baada ya Yondani kuambaa na mpira na kuachia shuti kali lililotoka nje kidogo ya lango huku pia wakifanya shambulizi lingine zuri dakika ya 79 baada ya Ibrahim Ajib kupiga faulo lakini mpira wa kichwa uliomaliziwa na Obrey Chirwa ulitoka nje.