Chelsea ina kazi ya ziada – Sarri

Muktasari:

  • Matokeo hayo yamemchanganya Kocha wake Maurizio Sarri, ambaye amesema timu hiyo inakabiliwa na kazi nzito ili kutimiza lengo la kutwaa ubingwa huo.

London, England. Kampeni za Chelsea kutwaa taji la Ligi Kuu England msimu huu zimepunguzwa kasi, baada ya kulazimishwa sare ya bila mabao na West Ham jana isiku.

Matokeo hayo yamemchanganya Kocha wake Maurizio Sarri, ambaye amesema timu hiyo inakabiliwa na kazi nzito ili kutimiza lengo la kutwaa ubingwa huo.

Uamuzi wa Sarri kuwapumzisha nyota wake kadhaa katika mchezo wa Europa Ligi, uliofanyika katikati ya wiki iliyopita akiwemo mpishi wa mabao Eden Hazard, ili waishukie West Ham haukusaidia kitu.

“Tumebadilika sana kwenye safu ya ulinzi, hivi sasa tunamudu kuzima mashambulizi lakini bado tuna tatizo kwenye ushambuliaji hatujaweza kuwa wabunifu tunapocheza na timu zinazojilinda zaidi,” alisema Sarri.

Alisema katika mchezo huo walitawala mchezo lakini tatizo likawa na kukosa mbinu za kupenya ili wafunge mabao, huku akisema hawezi kumnyooshea kidole mchezaji yeyote.

Sare hiyo imeifanya Chelsea kufikisha pointi 16 sawa na Manchester City lakini ikizidiwa kwa wastani wa mabao, huku Liverpool ikiendelea kukaa kileleni kwa kufikisha pointi 18.