Chelsea yazifanyia fujo United, Spurs

Muktasari:

  • Baada ya kusikia aliyekuwa beki wake Nathan Ake, anahitajiwa na Manchester United na Tottenham, klabu ya Chelsea imepanga kutumia sehemu ya kipengele cha mkataba cha kulipa mara dufu dau la mauzo, kumrejesha beki huyo anayekipiga Bournemouth,

London, England. Klabu ya Chelsea ni kama inazifanyia fujo Manchester United na Tottenham zilizokuwa zinamtaka beki chipukizi wa Bournemouth, Nathan Ake.

Chelsea imetoa ofa ya Pauni 40 milioni kumrejesha kikosini Ake iliyemkuza na kumpeleka Bournemouth kwa mkopo kabla ya kumuuza jumla Julai mwaka jana kwa Pauni 20 milioni.

Ake mwenye miaka 23 raia wa Uholanzi amekuwa tegemeo kwa Bournemouth jambo lililozivutia Man United na Tottenham na kutuma maskauti kumtizama kabla hazijawasilisha ofa.

Hata hivyo kujitosa kwa Chelsea iliyomlea tangu mwaka 2011 hadi 2017 ni wazi kutazitibulia timu hizo zilizomuhitaji kwani katika hali ya kawaida mchezaji huyo lazima atapendelea kurudi Stamford Bridge ambako amejipatia marafiki wengi.

Kubwa zaidi ni kuwa katika mkataba Chelsea, ilitakiwa kuipa Bournemouth fedha mara dufu ya ilizomuuza ikiwa itataka kumrudisha beki hiyo jambo ambalo wapo tayari kulitekeleza.

Aidha inaonekana kama Chelsea wanajaribu kumpiga vita kimya kimya kocha wao wa zamani Jose Mourinho, ambaye alifanya kazi na kinda huyo kabla hajatimuliwa Stamford Bridge, akiamini atafiti zaidi ya Eric Bailly na Victor Lindelof.

Naye kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino, anataka kumsaka mbadala wa beki wake Toby Alderweireld raia wa Ubelgiji ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni na anasita kusaini mkataba mpya.

Inahisiwa kuwa beki huyo hataki kusaini mkataba mpya kutokana na kupata mchongo kwenye timu nyingine kubwa za ndani au nje ya England.