Dabusi Fc yatwaa ubingwa Gidabuday Cup

Muktasari:

  • Katika mchezo huo mabao ya Dabusi yakifungwa na Yasini Zuberi kwa mkwaju wa penalti, huku bao la pili alijifunga beki wa Nangwa, Jackson Jolwa kabla ya Deograsia John kumalizia bao la tatu. Wakati mabao ya Nangwa yalifungwa na Nathan Matembo kwa mkwaju wa penalti na Gift Oscar.

Timu ya Dabusi imetwaa ubingwa wa mashindano ya Gidabuday Cup kwa kuichapa Nangwa kwa mabao 3-2 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwa VTC Wilayani Hanang’.

Katika mchezo huo mabao ya Dabusi yakifungwa na Yasini Zuberi kwa mkwaju wa penalti, huku bao la pili alijifunga beki wa Nangwa, Jackson Jolwa kabla ya Deograsia John kumalizia bao la tatu. Wakati mabao ya Nangwa yalifungwa na Nathan Matembo kwa mkwaju wa penalti na Gift Oscar.

Michuano hiyo iliyoanza Septemba tatu kwa kushirikisha timu tisa ilikuwa na lengo la kumpongeza katibu mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday kwa juhudi anazozifanya kwenye michezo hapa nchini.

Mgeni rasmi katika mchezo huyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Sara Ally aliwasihi vijana kupenda michezo kwa kuwa ni ajira nzuri.

“Asilimia kubwa ya pato la nchi kwenye mataifa yaliyoendelea yanachangiwa na wanamichezo na hata ukifuatilia watu wenye vipato vizuri katika ulimwengu wa sasa ni wanamichezo hivyo hupashwi kukata tamaa kama umeweka malengo ya kufika mbali kwenye soka” alisema Bi Sara.

Katibu msaidizi wa soka Wilaya ya Hanang’ Hosea Laja alisema kuwa michuano hiyo pia imesaidia vijana kukusanyika pamoja na kuongeza ushindani wa soka wilayani humo hasa kwa wale vija wasiokuwa na timu maalumu.

Timu zilizoshiriki katika michuano hiyo ni pamoja na Nangw VTC, Dabusi, Nangwa Milimani, Endamanack, Ngorongoro na Filuk zote kutoka kata ya Nangwa, Sagong na ANTSI kutoka kata ya Measkron huku kata ya Wareta ikitoa timu ya Getak pekee.