Dakika 90 zinasubiriwa

Muktasari:

Yanga na Simba ziko ugenini leo kupeperusha Bendera ya Tanzania katika michuano ya klabu Afrika.

Port Said, Misri/Dar. Unaweza kusema zinasubiriwa dakika 90 kwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika, Yanga na Simba.

Yanga iko nchini Botswana kurudiana na Township Rollers mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba itacheza na Al Masry mjini Port Said, Misri, mechi ya Kombe la Shirikisho.

Simba ilivyojipanga

Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre amefanya uamuzi mgumu kuelekea kwenye mechi hiyo na kama mambo yatakwenda vizuri basi Wanamsimbazi hao watacheeka.

Kwanza, Lechantre amemwondoa kwenye kikosi cha kwanza winga machachari zaidi wa timu hiyo, Shiza Kichuya ikiwa ni moja ya mbinu za kuwamaliza Waarabu hao ndani ya dakika 90 tu.

Lechantre ameiambia Mwananchi hapa Port Said, Misri kuwa amemvuta beki Mganda, Juuko Murshid ambaye atasimama na Mghana, James Kotei kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo la kiungo ili kuwadhibiti Waarabu hao wasicheze kabisa.

Pia, Lechantre alisema baada ya sare ya 2-2 mchezo wa kwanza, hesabu zake ni kucheza kwa kujilinda kwa dakika 60 kisha wafanye mashambulizi ya nguvu katika dakika za mwisho na kumaliza kwa ushindi.

“Tumetazama mechi kadhaa za Al Masry, hasa mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu hapa. Wanacheza vizuri mwanzo na wanakaba kila eneo. Ukiweza kuwazuia wasikufunge mpaka dakika ya 60 wanachoka, inakuwa rahisi kuwamaliza,” alisema Lechantre.

“Kutokana na hilo tutacheza kwa kujilinda zaidi mwanzoni mwa mchezo. Nimemwongeza Kotei kwenye kiungo na atacheza upande wa Kichuya. John Bocco na Emmanuel Okwi wataongoza mashambulizi safu ya mbele.

“Endapo tutamaliza dakika 60 bila kuruhusu bao basi ninaamini tutashinda. Ikifika muda huo nitaweza kumpa Kichuya nafasi pengine na Laudit Mavugo ili kucheza mipira ya juu na chini yenye uhakika,” alisisitza.

“Napata moyo kwamba tunaweza kushinda, wachezaji wamefanya vizuri sana kwenye mazoezi ya jana (juzi Alhamisi), wanaonyesha nia ya kupambana na wana hamu ya kushinda,” aliongeza kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika Kaskazini na Asia.

Okwi ajiamini

Rekodi tamu ya straika wa Simba, Emmanuel Okwi dhidi ya timu za ukanda wa Afrika Kaskazini imemfanya asiwe na presha yoyote kuelekea kwenye mechi ya leo jioni dhidi ya Al Masry ambapo amedai kuwa watapambana hadi tone la mwisho.

Okwi ambaye ameifungia Simba mabao 19 kwenye mashindano yote msimu huu, alisema anafahamu kuwa ana mzigo mzito kuelekea kwenye mechi hiyo hivyo atapambana ili kufanya vizuri.

Staa huyo ambaye bao lake la ugenini dhidi ya Es Setif ya Algeria lilibeba Simba mwaka 2012, alisisitiza kuwa kama kila mchezaji atacheza vizuri basi nafasi ya kushinda iko upande wao.

Baridi kali

Simba italazimika kucheza kwenye hali ya baridi ambayo usiku hushuka hadi nyuzijoto 15 lakini straika wao, Juma Liuzio anaamini kuwa kwa siku mbili walizokaa hapa walau kutakuwa na nafuu.

“Baridi ni kali sana, ni afadhali tumewahi, hata ingewezakana kuwahi zaidi ingekuwa jambo jema. Ila kwa siku hizi mbili tunaweza kuwa fiti,” alisema.

Kutokana na hali ya baridi, viongozi wa Simba walipanga kufanya manunuzi ya makoti ya ziada kwa wachezaji watakaokuwa benchi ili waweze kuwa kwenye hali nzuri.

Wachezaji wa Simba pia wengi wao walipewa tahadhari ya kubeba vifaa vya kuzuia baridi kama glovu na fulana za mikono mirefu ambazo wanaweza kuvaa ndani ya jezi zao.

Yanga wana hesabu kali

Hesabu za Yanga kuibuka na ushindi muhimu ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana zimekamilika huku wawakilishi hao wakitoa ahadi kuzitumia kikamilifu dakika 90 za mechi hiyo.

Rollers na Yanga zinarudiana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Gaborone saa 10.45 jioni baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 2-1.

Yanga inasaka ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili ifuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo ambayo kila timu itakayofanikiwa kuingia, itapata kitita cha Dola 550,000 (zaidi ya Shilingi 1.2 Bilioni) kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Endapo Yanga itapoteza mchezo huo, itashuka Kombe la Shirikisho Afrika na kuingizwa kwenye kapu la mechi za mchujo kisha itaingia makundi endapo itapita.

Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Samuel Lukumay, alisema jana kutoka Gaborone kuwa maandalizi na mazoezi ambayo timu hiyo imeyafanya kwa siku nne nchini Botswana yamewapa matumaini ya kuibuka na ushindi.

“Mazingira ya timu kuelekea mchezo wetu dhidi ya Township Rollers ni mazuri, benchi la ufundi limewaandaa vizuri wachezaji kiufundi, mbinu na kisaikolojia kwa ili waweze kuwapa furaha mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wa wachezaji morali na hamasa yao iko juu na wameahidi kupigana kufa na kupona ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi ambao utatuwezesha kufuzu hatua ya makundi.

Kimsingi kama viongozi tumetimiza majukumu yetu yote na kilichobaki ni kumuomba Mungu ili wachezaji waweze kumaliza kazi uwanjani,” alisema Lukumay.

Juzi vyombo vya habari vya Botswana vilimnukuu Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina akisema silaha kubwa ambayo timu yake itaitumia kwenye mchezo huo ni kutoingia kwenye mtego wa kufuata mbinu na staili za wapinzani wao.

Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini, wenyeji Township Rollers wanaonyesha bado hawajiamini na wamekuwa na lundo la mikakati ya kuhakikisha hawapotezi mchezo huo muhimu nyumbani.

Kwa mujibu wa mitandao ya kijamii ya Rollers, tiketi za mchezo huo zilianza kuuzwa tangu Jumatatu na hadi jana asubuhi, asilimia 65 ya tiketi zote zilikuwa zimenunuliwa lakini pia klabu hiyo ilitoa tiketi 200 za bure kwa wanafunzi wa shule.