Dante aanza mazoezi kuiwahi St Louis

Muktasari:

  • Yanga wanakutana na St Louis kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mechi itakayopigwa Jumamosi.

BEKI Andrew Vincent wa Yanga, alikosekana katika michezo miwili mfululizo ya timu hiyo kutokana na majeruhi yanayomsumbua, lakini mchezaji huyo ameanza mazoezi mepesi yeye mwenyewe akijiweka fiti kwaajili ya mechi ya Jumamosi.

Aliliambia Mwanasposti, aliumia akiwa yupo kambini Iringa hivyo ilimlazimu kukaa nje ili tatizo lake lijulikane, baada ya kwenda hospitali madaktari wamemuambia kwamba tatizo lake lilikuwa dogo hivyo aanze mazoezi mepesi.

“Nilikuwa najua nimechana nyama za paja, lakini madaktari wamenambia kwamba ni misuli tu ndio nimeshtua, nimeona bora nifanye mazoezi mepesi mwenyewe ili niendelee kujiweka fiti badaa ya kukosa michezo hii miwili,” alisema.

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya St Louis unaotarajiwa kupigwa Jumamosi, alisema mchezo huo una maana kubwa sana kwao hivyo wanahitaji kutoka na ushindi wa aina yoyote ili waweze kujiweka katika sehemu nzuri.

“Tupo nyumbani tunatakiwa tupate ushindi ili tuweze kujiweka katika sehemu nzuri ya Mashindano haya, mechi itakuwa ni ngumu lakini naamini pointi zote tutachukua na hawatoondoka na pointi zozote hapa nyumbani,” alisema.