Carragher aukubali muziki wa De Bruyne

Muktasari:

Kiungo huyo Mbelgiji amekuwa na msimu mzuri ndani ya kikosi cha Man City

London, England. Jamie Carragher amempa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka England, kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne.

Nguli huyo wa zamani wa Liverpool na England, aliseam De Bruyne ana sifa ya kuwa mchezaji bora wa kigeni England kutokana na mchango wake Man City.

Mchambuzi huyo wa soka alisema ingawa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji hakucheza mechi nyingi, lakini ana tuzo mkononi.

Carragher mmoja wa mabeki bora wa zamani wa England, alisema De Bruyne utampenda kwa mashuti makali ya mguu wa kushoto.

Hata hivyo, ubashiri wake umepingwa na manahodha wa zamani wa England, David Beckham na Steven Gerrard.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola amempa De Bruyne fursa ya kuonyesha uwezo wake katika eneo la kiungo mshambuliaji ambalo amelitendea haki msimu huu akicheza mechi 16 za mashindano tofauti.

“Tayari ana tuzo ya mchezaji bora wa mwaka hata kama amecheza mechi 12 au 13. Amefunga mabao manne msimu huu matatu kwa mguu wa kushoto, utamsimamisha vipi mtu wa aina hiyo ndani ya eneo la hatari,” alisema nguli huyo.

Mashuti ya De Bruyne, yanafananishwa na Beckham na Gerrard waliokuwa hodari kwa kufunga mabao kwa kufumua mikwaju ya mbali.

Mchezaji huyo alifung bao maridadi kwa shuti la mbali katika mchezo walioshinda mabao 2-0 dhidi ya Leicester City, Jumamosi iliyopita.