Djokovic, Federer hapatoshi fainali leo

Cincinnati, Marekani. Wachezaji nyota namba moja wa zamani wa tenisi duniani, Novak Djokovic na Roger Federer, leo wataonyeshana kazi kwenye fainali ya Cincinnati Masters.

Wachezaji hao waliowahi kushika namba moja kila mmoja kwa wakati tofauti, walitoana jasho katika nusu fainali ya mashindano hayo mwaka 2015, ambapo mashabiki walipata burudani ya uhakika kwani walitumia zaidi ya saa mbili kumka mshindi.

Novak Djokovic atakuwa akipigania kuandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda michezo yote tisa ya Masters 1,000, iwapo atatwaa taji hilo la Cincinnati Masters.

Nyota huyo kutoka Serbia, ambaye mara tano aliwahi kushika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo alimshinda Marin Cilic wa Croatia katika nusu fainali kwa 6-4 3-6 6-3.

Naye Federer, aliingia kwenye fainali baada ya mpinzani wake David Goffin wa Ubelgiji kuumia bega na kuamua kujitoa mashindanoni, hata hivyo wakati akijitoa walikua sare wakifungana seti 1-1.