Duh! Yaani Simba kama vile haipo

Muktasari:

Simba inacheza na Mbao FC leo Alhamisi Uwanja wa CCM Kirumba mechi ambayo ni mwendelezo wa michezo ya Ligi Kuu Bara.

Mwanza. Leo Alhamisi saa 10:00 jioni, mabingwa watetezi Simba watakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kukipiga na Mbao  FC, mchezo ambao ni wa Ligi Kuu Bara,  lakini hali ilivyo sasa si shwari kabisa.

Simba ni wageni katika mechi hiyo,  tangu wafike juzi Jumanne katika hoteli ya Lenana iliyopo Pasiansi, Wilaya ya Ilemela na kufanya mazoezi yao CCM Kirumba kimwonekano ni kama vile haipo kutokana na ukimya wao.

Inaonekana kama vile Simba wana hofu na mchezo huo kutokana na matokeo yao ya msimu uliopita ambapo walitoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Mbao kwenye uwanja huo.

Mbao imekuwa timu ambayo ikicheza na Simba inaonyesha kiwango bora na mara kadhaa wanautumia vizuri uwanja wao wa nyumbani tofauti na wanapokuwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa.

Imezoeleka kuwa Simba inapokuwa mikoani huwa inasindikizwa na mashabiki wao ambao huwa na furaha zinazotokana na kujiamini ni tofauti na ilivyo sasa jijini Mwanza.

Katika mechi iliyopita ya Ngao ya Jamii waliyocheza na Mtibwa Sugar katika uwanja huo, mashabiki walifika uwanjani mapema  huku shamrashamra zikianza mapema kabisa.

Inawezekana pia, huenda hali hii inachangiwa pia mchezo huo  kuchezwa katika ya wiki siku ambayo watu wengi wapo kazini ama bado hawajiamini nini kitatokea ndani ya dakika 90.