Erasto Nyoni aipa saluti Arusha United

Muktasari:

  • Erasto aliyechipukia kisoka mkoani Arusha akiwa chini ya Kituo cha Michezo ya vijana cha Rolling Store, alisema kuwa kurudi kwa hadhi ya kimichezo Arusha kutarudisha wachezaji wa mkoa huo wanaotapatapa mikoani kusaka timu

Arusha. Beki mkongwe wa Wekundu wa Msimbazi, Simba, Erasto Nyoni amesema kuwa kiwango walichokionyesha wachezaji wa Arusha United katika mchezo wao wa kirafiki ni dhahiri hadhi ya soka katika mkoa huo uko mbioni kurudi.

Erasto aliyechipukia kisoka mkoani Arusha akiwa chini ya Kituo cha Michezo ya vijana cha Rolling Store, alisema kuwa kurudi kwa hadhi ya kimichezo Arusha kutarudisha wachezaji wa mkoa huo wanaotapatapa mikoani kusaka timu.

“Kukosekana kwa amsha amsha ya soka Arusha ndio kunaua vipaji vya soka kutokana na baadhi wenye nia na malengo ya kucheza soka kukosa timu za kuchezea mkoani hapa hivyo kuanza kutanga tanga mikoani kusaka penye kufanikisha ndoto zake”

Nyoni alisema kuwa ukosefu wa timu ya Ligi Kuu ingawa ndio chanzo kikubwa kinachowakosesha vijana wa Arusha wenye vipaji kukosa ajira lakini pia hamasa ya viongozi na kiu ya kutamani kuwa na Ligi Kuu inachangia

“ Ujio wa timu hii ya Arusha United unaonesha sasa Arusha kuna matumaini ya kurudi kisoka na kuokoa vijana wanaotanga tanga huko mikoani kutafuta pa kujiegeza hivyo basi niwaombe viongozi wangu wa soka hapa wahakikishe wanapata timu ya Ligi Kuu kwa kuanzia na hii ambayo tumecheza nayo maana inaonekana mwanga mbele yao”

Simba ilikuwa Arusha kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Arusha United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara hali ambayo inatarajia kupata ushindani mkubwa dhidi ya timu ya ndugu zao Arusha FC wanaowakilisha mkoa huu

Mwenyekiti wa soka mkoa wa Arusha, Peter Temu akizungumzia ujio wa Simba Arusha alisema kuwa ni hamasa kwa wadau wa soka kusapoti timu za Arusha kuhakikisha wanapata burudani kama hiyo kila mara

“Sisi tunafurahia ujio wa timu kama hizi maana zinatusaidia kurudisha hamasa ya mpira Arusha na kuwaongezea wadau kiu ya kusapoti timu kupata burudani hizi mara kwa mara tofauti na sasa wanapata kwa kipimo”