Everton yamtaka Samir Nasri

Muktasari:

  • klabu ya Everton ambayo haijaonyesha cheche za kutosha katika Ligi Kuu England msimu huu, imepanga kumsajili kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa Samir Nasri ili kukiongezea nguvu na kukiimarisha kikosi chake.

Liverpool, England. Klabu ya Everton imepanga kumsajili kiungo wa zamani wa Arsenal na Manchester City raia wa Ufaransa, Samir Nasri.

Everton imeumizwa na kiwango duni ilichoanza nacho msimu huu na kocha Marco Silva anaamini akimpata kiungo huyo utakuwa ukombozi mkubwa kwake.

Amemfagilia Nasri akisema ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa licha ya kuwa nje ya dimba kwa muda kutokana kukumbwa na kadhia ya matuzimi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Kuanzia mwezi ujao Nasri atakuwa huru kujiunga na klabu yoyote kwani mkataba wake na klabu ya Antalyaspor ya Uturuki, utakuwa umemalizika rasmi wakati akimalizia kifungo chake cha masuala ya soka. 

Nasri alibainika kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni na Desemba mwaka 2016 akiichezea Sevilla ya Hispania kwa mkopo kutoka City, alipatiwa matibabu ya dawa hizo katika hospitali moja nchini Marekani.

Hata hivyo Nasri, alibainika kuendelea kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni jambo lililoikera klabu ya Antalyaspor na kuamua kuachana naye, ingawa Nasri hakutaka kusaka timu haraka akitaka kujiweka fiti kwanza.

Wakala wa kupambana na dawa zilizopigwa marufuku michezoni (Wada) imesema matumizi ya dawa hizo limekuwa janga la Dunia nzima na kuiomba jamii iunge mkono vita hiyo.  

Kocha Silva anataka Nasri mwenye miaka 31 awaongezee uzoefu wachezaji wake wa kiungo Richarlison na Gylfi Sigurdsson.

Wakati Ligi Kuu England ikiwa katika mzunguko wa nane, Everton inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 12 nane nyuma ya vinara Manchester City, Chelsea na Liverpool.