Fully Maganga anolewa kijeshi Dar!

Muktasari:

Maganga yupo jeshini anasoma kwa miezi minne na sasa yuko katika hatua za mwisho kumaliza, amepata nafasi hiyo akitokea kwenye klabu yake ya Ruvu.

UNAMKUMBUKA straika Fully Maganga aliyesumbua sana kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na klabu  ya Mgambo Shooting ya Tanga kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao, basi bwana kwa sasa  jamaa yupo jeshini anaongeza vyeo lakini amesisitiza, atakaporudi tu, ni kupiga mabao kama kawaida.

Maganga ambaye ni mwanajeshi na amesajiliwa na kikosi cha Ruvu Shooting, alipata nafasi hiyo ya masomo ya jeshi kwa mara nyingine kwa ajili ya kuongeza vyeo.

"Ukimya ni kwa sababu niko masomoni jeshini, naongezaa vyeo kwanza nikirudi uraiani niko vizuri. Kwenye mpira sijaonekana kabisa safari hii tangu ligi ilipoanza kwa sababu ya haya masomo, niliishia kusaini tu ndiyo nikaja huku,"anasema Maganga ambaye kozi anayosoma ni ya miezi minne maendeo ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.

"Kozi yangu ni ya miezi minne na sasa niko katika hatua za mwisho kumaliza, naomba Mungu nimalize salama, nirudi kuisaidia timu yangu ya Ruvu."