Gareth Bale anukia Old Trafford

Sunday November 19 2017

 

London, England. Manchester United bado ina dhamira ya kumsajili kiungo wa pembeni wa Real Madrid, Gareth Bale, ambaye anapitia katika wakati mgumu kwenye klabu hiyo.

Awali, Man United ilidai haina mpango wa kumsajili mchezaji huyo kwa kuwa amekuwa akiandamwa na majeraha ya muda mrefu.

Kocha wa Man United, Jose Mourinho amedai anaweza kumsajili nyota huyo wa Wales mwishoni mwa msimu. Mourinho anafuatilia kwa karibu maendeleo ya nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs.

Bale ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa wiki sita, baada ya kuumia tena wakati akikaribia kurejea dimbani akitokea katika majeraha.

Mourinho amekuwa na uhusiano mzuri na Bale tangu akiwa kocha wa Real Madrid kabla ya kutimkia Chelsea na baadaye kutua Man United. Man United iliwahi kumtupia ndoano mchezaji huyo mwaka 2013 akiwa Spurs kabla ya kuzidiwa kete na Real Madrid iliyomnunua kwa bei mbaya Pauni 85 milioni.

Mchezaji huyo mwenye miaka 28, amecheza mechi tisa msimu huu na hajacheza tangu Septemba 26 baada ya kupata maumivu makali ya kifua na misuli.

Winga huyo anataka kubaki Real Madrid kwa kuwa ana mkataba unamfunga hadi mwaka 2022, lakini amekuwa katika mazingira magumu na klabu hiyo inafikiria kumpiga bei.

Advertisement