Giroud aapa kupigania namba Chelsea

Muktasari:

  • Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Olivier Giroud amesema anayafurahia maisha katika jiji la London, hivyo hafikirii kuihama Chelsea kwa sasa licha ya kukumbwa na changamoto ya kukosa mabao, badala yake atabaki na kuboresha kiwango chake cha ufungaji mabao ili kupigania namba katika kikosi cha kwanza.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Olivier Giroud, amesema hafikirii kuihama timu yake ya Chelsea kwa sasa licha ya kutojihakikishia namba.

Giroud alisema atakachokifanya ni kujitahidi kuzitumia nafasi atakazozipata kufunga mabao kwani amekuwa na furaha ndani ya timu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge.

“Kwa hakika mimi sifikirii kuihama Chelsea kama inavyovumishwa kwa sababu ya kutokuwa na namba ya kudumu, nitabaki na nitajitahidi kufunga mabao ili nimshawishi kocha aniamini na kunipa nafasi zaidi,” alisema.

Mshambuliaji huyo ameyaweka wazi hayo kutokana na kuenea kwa tetesi kuwa anataka kuihama Chelsea aliyojiunga nayo mwaka jana akitokea Arsenal pia ya mji wa London na kurudi Ufaransa.

Alikiri kuwa na presha kutokana na kutofunga mabao lakini akasema hilo pekee haliwezi kumshinikiza kuondoka badala yake linamsukuma kujituma zaidi kufanya mazoezi ya kufunga.

Giroud amekuwa akihusishwa na mpango wa kurejea Ufaransa ambako anahitajiwa na timu ya Marseille.