Grobbelaar: Liverpool iliniokoa kuwa muuaji

Muktasari:

  • Asema kila akikumbuka mauaji aliyoyafanya ….

London, England. Kipa wa zamani wa Liverpool, Bruce Grobbelaar, amesema anashukuru kusajiliwa na timu hiyo kwa kuwa ilimuokoa kuwa muuaji.

Grobbelaar, 60, mzaliwa wa Zimbabwe, aliyasema hayo wakati akizungumzia vita ya msituni alivyovishiriki katika Taifa lake enzi hizo ikiitwa Rhodesia, katika miaka ya 1970 ambapo alisema kila akikumbukia moyo unamuuma.

Kipa huyo aliyeidaki Liverpool mechi 440 akitwaa mataji 13 katika miaka 13 aliyoidaki timu hiyo, alisema anakumbukia jisni alivyolazimishwa kumuua adui yake vitani.

“Ni tukio nililolifanya muda mrefu uliopita, lakini limekuwa likirudia akilini mwangu kama vile nimelifanya jana, huwa linaniogopesha kila ninapolikumbuka,” alisema Grobbelaar.

Alifafanua kuwa alishiriki kwa miezi 11 vita hivyo vya msituni vilivyopiganwa kati ya waafrika weusi waliokuwa wakipinga kutawaliwa na wazungu wachache katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.

Aliongeza kusema kuna wakati alikuwa akitamani hata kujiua yeye mwenyewe kila alipokumbuka namna alivyowashuhudia marafiki zake watatu wakiuawa na kilichomuokoa ni kitendo cha kutua Anfield.

“Kutua Anfield kuliweza kunisahaulisha mauaji yale kwani kabla ya hapo kuna wakati nilikuwa nikiweweseka usiku na picha ya mauaji ikinijia upya, hiki kilikuwa kipindi kigumu sana maishani mwangu.

Kabla ya kutua Anfield, Grobbelaar alicheza soka katika klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada mwaka 1979, Southampton na Plymouth na Kocha wa Liverpool, Bob Paisley alimuona wakati akicheza kwa mkopo Crewe kutoka Whitecaps na kuamua kumsajili.

"Nakumbuka kutua kwangu Liverpool kulitokea siku nilipoichezea Crewe dhidi ya York City ambapo Kocha Bob Paisley na Tom Saunders walikuja kuuangalia mechi hiyo ndipo wakaniona,” alisema na kuongeza.

“Kocha wangu aliniambia kuwa makocha hao wameridhishwa na uwezo wangu na wameapa lazima watanisajili nikacheze Uingereza, sikumuamini lakini baadaye ikawa kweli waliomba ruhusa kwa viongozi nikazungumza nao na nikasajiliwa na Liverpool,” alisema.