Guardiola kuwapumzisha saba

Muktasari:

  • City ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo la Ligi, watakuwa ugenini kuivaa Oxford huku ikiwapumzisha wachezaji saba kati ya wale walioanza mchezo wa ligi kuu juzi na kushinda 5-0 dhidi ya Cardiff.

London, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, amepanga kuwapumzisha mastaa wake saba katika kikosi kitakachoshuka dimbani kesho kuivaa Oxford United katika mchezo wa Carabao Cup.

City ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo la Ligi, watakuwa ugenini kuivaa Oxford huku ikiwapumzisha wachezaji saba kati ya wale walioanza mchezo wa ligi kuu juzi na kushinda 5-0 dhidi ya Cardiff.

Guardiola alisema sababu za kuwapumzisha wachezai hao ni kuwapa muda wa kukusanya nguvu kwa ajili ya mechi za ligi kuu, ikizingatiwa kuwa anakabiliwa na majeruhi watano.

Miongoni mwa wachezaji walio majeruhi ni Kevin de Bruyne, Claudio Bravo, Danilo, Eliaquim Mangala na Benjamin Mendy, ambao watakuwa nje kwa zaidi ya miezi miwili ijayo.

“Kuna baadhi ya wachezaji tumepanga kuwapumzisha katika mchezo dhidi ya Oxford kwa sababu tunawahitaji zaidi katika mechi za ligi kuu na pia kutoa nafasi kwa ajili ya chipukizi,” alisema Guardiola

City ambayo pia ni bingwa mtetezi wa ligi kuu, kwa sasa ipo nafasi ya pili ikizidiwa pointi mbili na vinra wa ligi msimu huu Liverpool iliyoshinda mechi zake zote sita za msimu huu.