Hanspope atuliza mizuka Simba

Muktasari:

  • Kwa misimu miwili Yanga imekuwa ikitoka nyuma na kuipiku Simba kutwaa ubingwa

Baada ya Simba kulazimishwa sare 2-2 na Mwadui, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo Zacharia Hanspope amewatuliza mashabiki na kuwaambia washushe presha kwani kikosi chao cha msimu huu kiko sasa na ubingwa ni lazima.

Mashabiki wa Simba waliondoka kimya kimya uwanjani baada ya Paul Nonga kuisawazishia Mwadui bao la pili dakika ya 89.

Pamoja na matokeo hayo Simba imeendelea kukaa kileleni kwa pointi 42 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 37, jambo linalowapa presha mashabiki wa timu hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo huo Hanspope alisema wala sare hiyo isiwape presha mashabiki kwani msimu huu ubingwa ni wao.

 “Unajua msimu huu tuna timu bora sana kwani tumesajili wachezaji wenye kiwango cha juu  kwa hiyo tusiwe na presha ya ubingwa kabisa na hii sare isitupe wasiwasi”alisema Hanspope kwa kujiamini.

Alisema sasa wanakwenda kujiandaa na mchezo wa marudiano wa kombe la Shirikisho Africa dhidi ya Gendarmarie Nationale ya Djibout.