Harry Kane aanza tambo World Cup

London, England. Muda mfupi baada ya kutangazwa nahodha, Harry Kane amesema England ina nafasi ya kutwaa Kombe la Dunia.

Kane alitoa tambo hizo timu hiyo ilipokuwa ikifanya mazoezi ya viungo baada ya kuingia kambini kujiandaa na fainali hizo.

Kocha wa England, Gareth Southgate, alimteua Kane nahodha mpya wa timu hiyo akiwapiku Jordan Henderson na Dyer.

Pia mshambuliaji huyo wa Tottenham Hotspurs, aliwataka wachezaji chipukizi kuwa jasiri na kujiandaa vyema kwa mashindano.

“Tunatakiwa kuwa jasiri haijalishi kama tutatupwa katika hatua ya makundi au nusu fainali, yote ni sawa,” alisema Kane.

Nahodha huyo alisema wachezaji wote walikubaliana kuondoa woga na kucheza kwa kujiamini kwa kuwa wana uwezo wa kushindana.

Alisema ndoto yake ni kuona England inashinda kila mchezo na ametoa wito kwa wachezaji kwenda kushindana kwa kuwa wanakutana na timu bora duniani.

Kinara huyo wa mabao katika Ligi Kuu England, alidokeza wanakwenda Russia kupambana katika fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 14.