BBC yatupiwa virago, yawageukia Hazard, Neymar safi

Muktasari:

Madrid msimu huu ipo katika hatari ya kupoteza taji yote iliyochukua msimu uliopita

 Madrid, Hispania. Real Madrid inawataka Neymar, Robert Lewandowski na Eden Hazard kuziba pengo la Karim Benzema, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo.

Rais wa Real, Florentino Perez lengo lake ni kufanya mabadiliko ya safu yake ya ushambuliaji mwisho wa msimu huu kwa mujibu wa taarifa za Hispania.

Washambuliaji hao watatu Benzema, Bale, Ronaldo (BBC) walikuwa na mafanikio makubwa katika misimu nne iliyopita wakitwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa kwa pamoja.

Hata hivyo kufanya vibaya kwa Real msimu huu kumemfanya rais wa Madrid kufikiria kufanya mabadiliko ya kikosi chake msimu ujao.

Ripoti kutoka gazeti moja maarufu la Madrid, Marca inadai Perez ana mafowadi watatu anaowataka kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao ni Neymar, Eden Hazard na Robert Lewandowski, akija kucheza namba 9.

Mastaa hao wa tatu kwa muda sasa wamekuwa wakiwindwa na wababe hao wa Hispania na imeripotiwa kwamba, dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi likifunguliwa tu Ulaya, basi kazi itakuwa moja tu kuhakikisha wanatua Bernabeu.

Real Madrid haijafanya usajili wowote mkubwa tangu walipomnasa James Rodriguez mwaka 2014, lakini sasa wamepanga kutumia pesa ili waendane na ushindani unaofanywa na Barcelona na PSG katika kipindi hiki.

Lakini, Rais wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon amesema klabu hiyo inavujisha makusudi taarifa za mastaa inaowataka ili kuwatuliza mashabiki ambao, kwa sasa hawafurahii kabisa na mwenendo wa timu hiyo kwenye La Liga.

Kwa madai ya Calderon ni kwamba kutajwatajwa kwa akina Neymar ni kiki tu zinazofanywa na uongozi wa timu ili kuwafanya mashabiki kuanza kuwajili mastaa hao badala ya mwenendo wa timu kwenye ligi.

"Hii ni mbinu ya Real Madrid ambayo wamekuwa wakiitumia kuwasahaulisha mashabiki kuhusu matatizo ya timu yao kwa kuwaahidi ndoto nyingi na kisha wanazivuruga ndani ya uwanja msimu ujao," alisema Calderon.