Joshua kuwanyoosha Wilder na Fury

Muktasari:

  • Ni baada ya kutwaa ubingwa wa IBF, WBO na WBA

London, England. Bingwa wa Dunia wa IBF, WBO na WBA uzani wa juu Anthony Joshua, amesema atafanya maandalizi ya uhakika ili kumshinda bondia yeyote atakayepangwa kucheza naye kati ya Deontay Wilder na Tyson Fury.

Joshua ametwaa ubingwa huo baada ya kumchapa kwa KO raundi ya saba Alexander Povetkin raia wa Russia katika pambano lililofanyika kwenye uwanja wa Wembley jijini London, Jumamosi usiku na sasa anasubiri kucheza pambano la kuunganisha mikanda ya IBF, WBO, WBA na WBC.

Mbabe huyo wa Uingereza mwenye asili ya Nigeria, anasubiri kucheza na bingwa mpya wa Dunia wa WBC atakayepatikana Desemba mosi mwaka huu baada ya mchezo kati ya mmarekani Deontay Wilder anayeutetea ubingwa wake dhidi ya Tyson Fury wa Uingereza.

“Baada ya kuvunja mwiko kwa kumpiga Povetkin nitajifua kwa nguvu zaidi ili niweze kumkabili bingwa yeyote atakayepatikana kati ya Wilder na Fury, sitarajii kupoteza mikanda yangu,” alitamba.

Kwa maana hiyo Joshua atapanda ulingoni Aprili mwakani ambapo atarudi kwenye uwanja ule ule uliompa heshima Jumamosi usiku kusaka taji linguine la dunia.

Iwapo Wilder na Fury kwa sababu zozote zile watashindwa kupanda ulingoni mpinzani anayefuatia katika pambano hilo la Aprili atakuwa mwingereza mwingine Dillian Whyte, anayeshilia nafasi ya kwanza kwa wapinzani katika mkanda wa WBC.

“Pambano la kuunganisha mikanda ya IBF, WBO, WBA na WBC litafanyika Aprili 13 mwakani tayari Joshua amethibitisha kwa kumshinda Povetkin kazi imebaki kwa Wilder na Fury," alisema mmoja wa maofisa wa WBC.