Wednesday, September 13, 2017

Julio aikubali kasi ya kocha msaidizi

 

By Matereka Jalilu

Kocha asiyeishiwa maneno Jamhuri Kiwhelo maarufu Julio ambaye anakinoa kikosi cha timu ya Dodoma FC kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ameonyesha kuukubali muziki wa msaidizi wake na kutamka kuwa timu pinzani zitakoma.

Julio mbali na kutamka maneno ya kumkubali msaidizi wake Muhamed Muya, pia amemtabiria makubwa kocha huyo ikiwemo kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa kutokana na ubora alionao ambao kwa kushirikiana naye anaamini wataipandisha ligi kuu timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Julio alisema ubora alionao msaidizi wake, timu pinzani kwenye kundi lao itabidi wateme mate chini kwani ni kocha mwenye uwezo mkubwa na kwamba ushirikiano wao umeifanya timu hiyo kukamilika kila idara na hakuna timu itakayowasumbua kwenye ligi hiyo.

“Siku zote napenda kuwa mkweli kwamba huyu msaidizi wangu ni bonge la kocha kiwango cha kuwa msaidizi wa timu ya taifa kutokana na mbinu zake ameifanya kazi yangu kuwa nyepesi kabisa imenipa jeuri ya kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu,” alisema Julio.

Julio aliongeza kuwa wamejiandaa vya kutosha na ili kudhihirisha maneno yake kuwa timu hiyo itapanda ligi kuu msimu ujao wataanza kwa kuifunga Pamba ya Mwanza kwenye mchezo wa kwanza wa ligi hiyo utakaochezwa Jumapili hii ili iwe salamu kwa timu nyingine zilizopo kundi moja.

Wakati huohuo katika kujiimarisha kiuchumi timu hiyo baada ya kutambulisha kikosi chao imeanza zoezi la uuzaji wa jezi rasmi za timu hiyo zilizotengenezwa nchini China kwenye mitaa mbalimbali mjini hapa na kilele chake kitakuwa Jumamosi.

-->