Kagera yafunga usajili kwa Athanas

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo alitamba akiwa na Stand United kabla ya kwenda Simba aliposhindwa kuonyesha ubora wake

Kagera Sugar imeendelea kuisuka safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili mshambuliaji Pastory Athanas ili kumaliza ukame wa mabao.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ameachwa na Singida United iliyomchukua kwa mkopo kutoka kwa vinara wa Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alithibitisha kuinasa saini ya nyota huyo na kwamba anaamini mapungufu kwenye ufungaji yatakwisha na kufanya vizuri.

Alisema kuwa usajili wa Athanas na Atupele Green wamefunga usajili wao na sasa wanaingia mawindoni kujiandaa na raundi ya pili.

“Tumempata Athanas anaungana na mwenzake Atupele kuitumikia Kagera Sugar, hatuongezi wala kupunguza mchezaji mwingine”alisema kocha huyo.

Meneja wa mchezaji huyo, Muhibu Kanu alisema kuwa anaamini Kagera Sugar ni sehemu salama Athanas kuonyesha kipaji chake na kuisaidia timu.

“Ameenda Kagera Sugar hadi mwisho wa msimu huu na baada ya hapo tunaweza kukaa chini na kusaini mkataba mrefu au awe huru kupokea ofa nyingine kutoka timu nyingine,”alisema Kanu.

Kagera ipo nafasi ya 10 kwa pointi 11 baada ya kushuka uwanjani mara 11,ambapo imeweza kufunga mabao saba na kuruhusu tisa kwenye nyavu zao.