Kambi Moro, Manji viliipa mzuka Yanga

Muktasari:

  • Yanga iliyofanya vibaya katika mechi nne za kwanza za michuano hiyo ikifungwa mara tatu na kutoka sare mmoja, imeshapoteza nafasi ya kutinga robo fainali lakini katika mechi ya juzi iliwashangaza wengi kwa kupiga soka la uhakika na kuwaacha na maswali yasiyo na majibu na kuibuka na ushindi huo.

Dar es Salaam. Ni wazi kambi iliyowekwa huko Bingwa nje kidogo ya mji wa Morogoro ni moja ya sababu za kufufuka kwa Yanga kufanya kwenye kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ilipoiduwaza USM Algiers ya Algeria, kwa mabao 2-1 mchezo uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga iliyofanya vibaya katika mechi nne za kwanza za michuano hiyo ikifungwa mara tatu na kutoka sare mmoja, imeshapoteza nafasi ya kutinga robo fainali lakini katika mechi ya juzi iliwashangaza wengi kwa kupiga soka la uhakika na kuwaacha na maswali yasiyo na majibu na kuibuka na ushindi huo.

Tangu mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji alipojiuzulu nafasi hiyo Mei mwaka jana, Yanga imekuwa haina mwenendo mzuri nje na ndani ya uwanja tofauti na kipindi cha kabla ya hapo.

Katika kipindi hicho chote Yanga haikuwa ikionyesha kiwango chake kilichozoeleka ikaaminika kuwa morari na hamasa kwa wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo iliyeyuka.

Kiwango hicho kibovu kilisababisha kuvuliwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu na watani zao wa jadi, Simba na kufanya vibaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika japo walibahatika kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuanza vibaya.

Kwa kiwango walichokionyesha juzi na Manji alikuwa jukwaani kuwashuhudia bila shaka wangecheza hivi katika mechi nne zilizopita leo wangekuwa wamefuzu ama wangehitaji sare kutinga robo fainali.

Kuna tofauti kubwa ilionekana katika mechi nne zilizopita Yanga iliambulia sare moja kufungwa tatu huku ikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11, wakati juzi ilifunga mabao mawili na kuruhusu moja ikivuna pointi tatu za kwanza.

Sababu za ushindi

Ujio wa Manji uwanjani na kambi ya Morogoro vimesaidia kupata ushindi huo, kama anavyobainisha Kocha msaidizi wa timu hiyo Noel Mwandila aliyesimama kwenye benchi katika mchezo huo badala ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera.

Alisema katika muda wote wa kambi yao Morogoro walikuwa wakiyachambua makosa yao na kuyafanyia kazi, pia upangaji wa kikosi, kumuweka langoni kipa, Beno Kakolanya, aliyemudu kuokoa mashambulizi ya hatari, kucheza mipira ya krosi na kona ilikuwa sababu nyingine ya ushindi.

Kuanzishwa kwa beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kucheza kiungo namba sita akisimama mbele ya mabeki Kelvin Yondani na Andrew Vincent waliocheza beki wa kati ilisaidia kuimarisha ulinzi kwani alianza kukaba kila waliposhambuliwa hivyo kuwapa mwanya mabeki wake kujipanga.

Kocha Zahera, alisema kuwa aliibadili timu hiyo kurudi kwenye soka lake la asili la kasi ambalo liliwasaidia katika mashambulizi na pindi walipokuwa wanashambuliwa walijilinda kwa pamoja na hata kuwapoteza waarabu katika ramani.

“Tulifanyia kazi makosa yetu katika mechi zilizopita ndio maana tunafahamu kufanya kosa sio kosa bali kurudia kosa ndiyo vibaya,” alisema.

Alisema jambo lingine alilofaulu ni wachezaji wa safu ya kiungo kuonyesha utulivu kwa kumiliki mipira, wakipiga pasi sahihi zilizowafikia walengwa na kila walipopoteza walirudi nyuma kusaidia kukaba.

Pia umahiri wa washambuliaji wakiongozwa na mshambuliaji mpya Herietier Makambo kutoka DR Congo aliyeonekana kujiamini na kujituma muda wote wa mchezo ilikuwa sababu nyingine iliyozaa matunda dhidi ya USM Algiers juzi.

Mbali na ubora wa uwanjani, mchezo huo wa juzi ni kama ulikuwa mwanzo wa kurudisha hamasa ya Yanga nje ya uwanja hasa ikichagizwa na kitendo cha Manji kwenda uwanjani na kushuhudia mchezo huo lakini pia mashabiki wake ambao awali walionekana kukata tamaa, walijitokeza kwa wingi na kuipa sapoti timu hiyo kuanzia dakika za mwanzoni hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.

Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alikiri kuwa uimara ulioonyeshwa na timu kwenye mchezo huo kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya kambi ya wiki mbili mkoani Morogoro pamoja na hamasa waliyokuwa nayo.

“Nadhani hatukuwa fiti siku za nyuma lakini tulipokuwa kambini tulijaribu kufanyia kazi kasoro ambazo tulikuwa nazo lakini tulihakikisha tunakuwa fiti kiasi cha kutosha zaidi ya vile tulivyokuwa.

“Lakini pia ingawa hatukufanya vizuri siku za nyuma, tulikubaliana kwamba japo hatukuwa na cha kupoteza kwenye mechi hiyo tuhakikishe tunapambana ili tulinde heshima yetu na kurudisha imani kwa mashabiki.

“Kwa bahati nzuri uongozi umekuwa pamoja na sisi kwenye maandalizi na mashabiki walijitokeza kwa wingi kutuunga mkono, jambo ambalo lilisaidia kuongeza morari kwa wachezaji,” alisema Mwandila.

Matokeo hayo ni mabaya kwa Waarabu hao kwani ushindi wa Rayon Sport iliyoichapa Gor Mahia 2-1 umefufua matumaini ya timu hiyo ya Rwanda kwani endapo itaifunga Yanga mchezo wa mwisho itafikisha pointi tisa na Gor ikishinda mchezo wake na waarabu hao, watakuwa wameaga na timu hizo za Cecafa zitakata tiketi ya kusonga mbele.