Kelvin wa Serengeti Boys apata ulaji Ulaya

Muktasari:

  • Kelvin Jonh amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Denmark ambapo atajiunga na timu ya Ligi Daraja la Kwanza HB Koge. Kinda huyo wa timu ya Taifa ya Serengeti Boys, anakuwa mchezaji wa pili kupata kufuzu majaribio ya kucheza soka nchini humu akitanguliwa na Morice Abraham.

Dar es Salaam. Mshambuliaji nyota wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Kelvin John, amesema haikuwa kazi rahisi kufuzu majaribio ya kucheza soka Ulaya.

Kelvin alikwenda kufanya majaribio ya wiki mbili kucheza soka la kulipwa katika kikosi cha vijana HB Koge ya Denmark.

Kinda huyo aliwasili nchini juzi akiwa ameongozana na msimamizi wa Kampuni ya Barass Sports Management Limited, Jamal Barass akitokea Denmark.

Kelvin alisema kuanza maisha mapya ugenini ilikuwa changamoto, lakini alipambana kuhakikisha anashinda majaribio hayo.

Mchezaji huyo alisema alikwenda Denmark akiwa na ndoto ya kucheza soka la kulipwa kwa kuwa aliamini ana uwezo wa kushindana na chipukikizi wengine kuwania nafasi hiyo.

“Baridi na vyakula vyao vilikuwa tofauti, lakini kwa upande wa soka hakuna tofauti kubwa ingawa wenzetu wameendelea zaidi. alisema Kelvin.

Akizungumza na gazeti hili jana, Jamal alisema kuwa wanatarajia kuanza mazungumzo na makocha wa HB Koge ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.

“Alikuwa kivutio kwa benchi la ufundi la timu yao ya vijana, walivutiwa na kasi yake pia namna anavyojua kucheza na nafasi, Kelvin ni mchezaji mzuri walikuwa wakilisema mara kwa mara,” alisema Jamal.

Kelvin ni kijana wa pili akitokea Serengeti Boys kufuzu majaribio nchini humo akitanguliwa na nahodha wake Morice Abraham ambaye amefuzu timu ya vijana ya Midtylland.

Nyota hao wanatarajiwa kuiongoza Serengeti Boys katika Fainali za Afrika (Afcon) zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania.

Kituo ambacho kimekuwa kikimlea, Kelvin cha ‘Football House’ kupitia mkurugenzi wake Mbaki Mutahaba kimetoa baraka kwa kinda huyo kwenda kucheza soka la kulipwa Denmark.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka (TFF), Ammy Ninje alisema Kelvin kufuzu majaribio ni taarifa njema ambayo anaamini kila Mtanzania anayependa maendeleo ya soka nchini atafurahi.

“Wanatakiwa kwenda wengine kwa manufaa zaidi ya Taifa letu, kwa mpira wa ushindani wa kisasa, unauhitaji mkubwa wa wachezaji ambao wamekomaa kiushindani na lazima wacheze kwenye ligi zilizoendelea.

“Kelvin bado umri wake ni mdogo ana muda mzuri wa kuendelea kujifunza vitu ambavyo vitamfanya kuwa mmoja wa wachezaji hatari siyo kwa Tanzania hata Afrika na duniani kote,” alisema Ninje.