Hakimu ashangaa miezi tisa upelelezi bado

Muktasari:

  • Malinzi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 28 ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi na utakatishaji wa fedha.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka umetakiwa kukamilisha upelelezi wa kesi inayowakabili viongozi wa watatu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haraka ili haki itendeke kwa washtakiwa hao wamekaa rumande kwa miezi tisa sasa.

Viongozi hao ni aliyekuwa Rais TFF, Jamal Malinzi (57), Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Mwanga(27).

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri aliyaeleza hayo leo na kuongeza kusema kuwa ni aibu na ajabu kwa upande wa mashtaka kwenda mahamani na kusema upelelezi bado haujakamilika.

"Ni miezi tisa sasa imepita bila ya upelelezi kukamilika washtakiwa wapo rumande, kinachotakiwa ni ukamilishwaji wa upelelezi wa kesi," alisema Hakimu Mashauri.

Hata hivyo aliyatupilia mbali maombi ya upande wa utetezi ya kuhusu kuwa na mamlaka ya kuwaachia washtakiwa chini ya kifungu cha 225, (5) cha sheria ya Mwendo wa makosa ya jinai.

Hakimu Mashauri alisema mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kuwaachia washtakiwa hao kwa sababu miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kughushi ambayo hayaingii katika kanuni ya ukomo wa Mashauri kukamilishwa ndani ya siku 60.

Kwa upande wa Wakili wa Malinzi na Mwesigwa, Kashindye Thabiti alilalamika mahakamani hapo kuwa wakienda magereza wanakosa uhuru wa wakuwaona wateja wao wakiwa mahabusu.

"Mheshimiwa hatuna haki ya kwenda kuwatembelea wateja wetu mahabusu, ukienda magereza unakataliwa getini hadi uende Makao Mkuu ya Magereza upate kibali ndiyo uweze kuongea na washtakiwa."Alieleza Kashindye.

Hivyo aliiomba mahakama iwasaidie waweze kupata oda kwa sababu wateja wao ni kama wagonjwa wanapomuona daktari wanapata nafuu, kitendo cha kukataliwa hawatendewi haki wao pamoja na wateja wao.

Wakili wa Serikali, Upendo Temu alieleza mahakamani hapo kuwa wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa na Magereza.

Wakili wa utetezi Abraham Senguji alidai wanaona hiyo  siyo haki na ni uvunjifu wa katiba tunaomba wakili wa Serikali atueleze kwa nini wanazuia tunaomba oda turuhusiwe kuwasalimia wateja wetu bila kikwazo chochote.

"Nashangaa hata katika kesi ya kawaida kama hii labda watueleze kuna kitu gani ndani ya chungu," Alieleza Senguji.

Wakili wa Serikali, Desa Olombe alieleza mahakamani hapo kuwa yeye haoni kama wamekatazwa ni utaratibu umetolewa upate kibali uonane na wateja wako.

Kila mahali pana utaratibu wake, magereza ndio wanawahifadhi washtakiwa, haki inaenda na wajibu na tunao wajibu wa kufuata utaratibu uliowekwa na wahusika, alieleza Olombe.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo,Hakimu Mashauri alisema katika kutembelea mahabusu wakiopo magereza ni lazima utaratibu ufuatwe.

Kesi imeahirishwa hadi Machi 28,2018 kwa ajili ya kutiwa.

Machi 8, 2018 upande wa utetezi ulilalamika mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imechukua muda mrefu ambapo washtakiwa wapo rumande kwa takribani miezi 8 sasa tangu walipofikishwa kwa mara ya kwanza mwezi Juni, 2017.

Kwa kipindi chote hicho upande wa mashtaka umeendelea kueleza mahakama upelelezi bado haujakamilika kwa madai kuwa DPP bado unaendelea kupitia jalada hilo.

"Sisi mawakili na wateja wetu hatuna malalamiko yoyote dhidi ya mahakama tunaelewa inafuata sheria na taratibu na mahakama haijapewa mamlaka ya kulazimisha upande wa jamuhuri useme upelelezi umekamilika.

Hivyo aliomba iwepo kwenye kumbukumbu za mahakama kuwa wao wanalia na ofisi ya DPP.

Wakili Nehemiah Nkoko alidai kuwa hati ya mashtaka ipo wazi ambapo inaonesha risiti na viasi vya fedha zinazodaiwa kuibiwa hivyo wanata kuambiwa ukweli ni kitu gani kinachokwamisha upelelezi katika kesi hiyo kukamilika.

Alidai kuwa wateja wao wapo ndani wanaumia na wanahitaji kujua hatma ya kesi yao kama kufungwa wafungwe na kama kuachiwa waachiwe.

Wakili Abraham Senguji ambaye pia ni wa upande wa utetezi alidai kuwa kwa namna hati ya mashtaka jinsi  ilivyo imejitosheleza na hivyo aliiomba mahakama iamuru upande wa mashtaka tarehe itakayopangwa wake na mashahidi kwa ajili ya kuisikiliza kesi hiyo.

Vinginevyo wapewe ahirisho fupi ili wawasilishe hoja kuhusiana na mwenendo wa upande wa mashtaka jinsi unavyoiendesha kesi hiyo na mahakama itoe uamuzi.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Swai alidai kuwa ombi la kuleta mashahidi ili kesi ianze kusikilizwa haliwezekani kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa wamekuwa wakiiharifu mahakama katika kila hatua ya upelelezi hivyo aliiomba mahakama isitoe amri kwa maombi yoyote ya upande wa utetezi.

Alibainisha kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo kwa DPPna kwamba hawana nia ya kuichelewesha kesi hiyo na akaomba wapewe siku 14 ili walifuatilia jalada la kesi hiyo.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29,2017, wakikabiliwa na mashtaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha dola za Marekani 375,418. 7

Katika kesi hiyo, Malinzi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 28 ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi na utakatishaji wa fedha dola za marekani 375,418.

Katika kesi hiyo Malinzi wanakabiliwa na mashtaka 28 huku wenzake wakikabiliwa na makosa yasiyozidi manne.

Wakati kesi hiyo ikitajwa washtakiwa wote walikuwapo mahakamani na wanateteWa na Mawakili  Nehemia Nkoko, Dominician Rwegoshora na Abraham Senguji.