Masogange asuburi hukumu tu

Muktasari:

Masogange katika kesi hiyo anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine)

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 21, 2018 itatoa hukumu katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili Video Queen, Agnes Gerald ‘Masogange’.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula kuwaita mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi ya Masogange na kuufunga na mshtakiwa mwenyewe kujitetea.

Akiongozwa na Mawakili Nehemiah Nkoko na Ruben Simwanza kutoa utetezi wake leo Masogange ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.

Masogange  anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam, katika utetezi wake amedai kuwa yeye hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja.

Akijitetea Masogange alidai kuwa mbali ya ‘Uvideo Queen’ pia alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo.

Alidai kuwa Februari 14,2017 polisi walienda nyumbani kwake, yeye hakuwepo, alikuwepo dada yake, yeye alikuwa amempeleka mjomba wake kununua vitu Ocadeco.

"Polisi waliniulizia, dada yangu aliwauliza nyie ni kina nani, wakamueleza kuwa wao ni ndugu zetu, dada yangu aliwaambia sisi hatua ndugu kama nyie", alieleza Masogange.

Alieleza kuwa polisi hao walimuweka chini ya ulinzi dada yake na kumtaka ampigie simu na ajifanye anaumwa ili arudi nyumbani.

Masogange alieleza kuwa dada yake alimpigia simu na kumueleza anaumwa sana, naye akamjulisha kuwa ataenda muda sio mrefu, lakini alikwenda saa 12 jioni.

Alidai kuwa ilipofika nyumbani kwake getini kabla hajashuka kwenye gari alimuona mlinzi amekaa na watu wanne, aliwasalimia na kuingia ndani.

Aliendelea kudai kuwa ilipofika ndani alimkuta dada yake, askari wa kike na askari wawili wa kiume, walimueleza wanasubiri yeye na wakajitambulisha kuwa wao ni polisi.

Masogange alidai kuwa aliwauliza wanashida gani na wakamueleza kuwa wamekwenda kufanya upekuzi, wakapekuwa wakamueleza kuwa hawatapata kitu chochote.

Alidai baada ya upekuzi huo, alichukuliwa na kupelekwa kituo kuu cha polisi na kwamba walipofika mapokezi akaandikisha jina na wakampeleka rumande ambapo alikaa siku tisa.

Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa Februari 14, 2017 na Februari 15, 2017 akiwa polisi alipelekwa katika ofisi iliyokuwa na watu 15 ambapo kwa nyakati tofauti alikuwa akimuuliza maswali.

Baada ya mahojiano, Masogange alidai kuwa alipelekwa Mwananyamala ambapo alioneshwa picha mbili za wanaume wawili, akaulizwa kama anawafahamu na kuwaeleza kuwa hawafahamu.

Alidai baada ya hapo alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo afande Judy alishuka katika gari walilokuwa nalo, akamuita mama wa makamo, akamuomba kikontena kidogo cha plastiki cha kuhifadhia mkojo na Masogange akaambiwa angozane na mama hiyo.

Aliendelea kudai aliongozana naye, wakaingia chooni ambapo huyi mama wa makamo alimkabidhi kikontena hicho cha kuwekea mkojo, akaingia chooni mwenyewe akatoa mkojo na kumkabidhi hiyo mama wa makamo .

Masogange alidai kuwa baada ya hapo afande Judy walimueleza hiyo mama wa makamo kuwa watawasiliana, na akarejeshwa polisi.

Masogange aliendelea kutoa utetezi wake alidai kuwa yeye hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja.

Alibainisha kuwa mtu anayetumia dawa za kulevya hawezi kuhimili kukaa siku bila ya kutumia dawa za kulevya utetemeka na kuwa kama amechanganyikiwa, lakini yeye alikaa na hali yake ikiwamo nzuri.

" Mheshimiwa mimi sijawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja nipo tayari hata mahakama yako ijiridhishe kwa kunipima." Alieleza Masogange.

Wakili wa Serikali, Kakula alimuuliza Masogange kuwa ni sahihi alikamatwa Februari 14,2017.

Masogange ni kweli

Kakula ni sahihi Februari 15,2018 ulipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali 

Masogange: kweli

Kakula uliongozwa na askari wa kike akiwa na chupa

Masogange hapana

Kakula ni sahihi huo mkojo ni wewe mwenyewe uliutoa na kumkabidhi yule mama wa makamo

Masogange: ndiyo

Masogange katika kesi hiyo anadaiwa kuwa kati ya February 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Pia, anadaiwa kuwa kati ya February 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.