Kibadeni: Wachezaji wakiliheshimu soka litawaheshimu uzeeni

Muktasari:

  • Amejitolea mfano yeye mwenyewe kuwa alitenga muda wa kuutumikia mchezo huo ndiyo maana unampa heshima mpaka leo kuendelea kula matunda ya kazi hiyo licha ya kwamba hachezi.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni amewashauri wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara kuuheshimu kazi yao itawaheshimu watakapokuwa wazee kama yeye.

Amejitolea mfano yeye mwenyewe kuwa alitenga muda wa kuutumikia mchezo huo ndiyo maana unampa heshima mpaka leo kuendelea kula matunda ya kazi hiyo licha ya kwamba hachezi.

"Kila mchezaji akijiuliza kwa nini baadhi ya majina ya wakongwe ndiyo yangang'ara mpaka sasa, watataka kufahamu kwamba walifanya nini, hilo litawasaidia kujituma kwa bidii ili na wao waje kupata heshima hiyo," alisema.

Amewageukia wale ambao wanacheza Simba na Yanga kwamba kuvaa jezi tu inawapa hatua ya jamii kuwajua wapo wapi, huku akiwasisitiza jambo la pili kuwa wazitendee haki ya kuonyesha uwezo uwanjani.

"Klabu hizo zinahitaji watu wenye uwezo wa juu na siyo mladi unavaa jezi zao bila uwezo, wajitume itasaidia hata timu ya Taifa Stars, kuwa kwenye kiwango cha juu," alisema Kibadeni.