Kichuya awafunika Kagere, Okwi Mwanza

Muktasari:

  •  Ni kawaida kila zinapocheza Simba na Yanga mikoani wafanyabiashara kuingiza fedha kwa mauzo ya jezi.  

Dar es Salaam. Kama mashabiki wa soka nchini wanadhani straika wao Meddie Kagere ndiye anafanya vizuri sokoni basi siyo sahihi, Shiza Kichuya ndiyo mpango mzima Simba.

Iko hivi.  Wafanyabiashara wa jezi za wachezaji mbalimbali nchini wamesema hivi sasa biashara kwao imekuwa ngumu kwani jezi pekee upande wa Simba inayofanya vizuri kwenye mauzo ni ya Kichuya tangu atue Msimbazi.

Azizi Msofe alisema mbali na Kichuya anayefuata kwa mauzo ndani ya Simba ni Emmanuel Okwi na Kagere.

"Biashara ni mbaya kwasababu Simba imetoka huku hivi karibuni kucheza mechi ya Ngao ya Jamii, mashabiki wa mikoani wana tabia ya kununua jezi siku ya kwanza yaani mechi moja tu ya kwanza na si vingine.

"Ila ukweli ndani ya Simba bado Kichuya ni kipenzi cha watu popote ninapokwenda yeye ndiye huuza zaidi kuliko wachezaji wengine," alisema Msofe

Mfanyabiashara aliyetambulika kwa jina la Dinonga Dinonga alisema, "Biashara ngumu ila tunaamini tukienda Shinyanga na Musoma tutauza kwani huko hawajawaona wachezaji wa Simba, ila kikubwa viongozi wa hizi timu wapunguze bei za jezi.

"Hapa kuna jezi za Sh 25000, 15000 na 10000, tunazunguka karibu nchini nzima na nchi jirani kwa ajili ya hii biashara ila kwasasa hapa Mwanza hakuna biashara na hii si kwasababu mechi unacheza siku ya kazi bali ni kwa vile Simba walikuja huku hivyo mashabiki hawana mzuka," alisema Dinonga.