Kiharusi chamlaza bingwa wa Olimpiki

Monday September 10 2018

 

Los Angeles, Marekani. Mwanariadha Michael Johnson, ambaye ni bingwa wa zamani mara nne wa Olimpiki wa mbio za mita 200 na 400, ameanza kupata ahueni baada ya kupatwa na kiharusi.

Johnson aliyeingia kwenye rekodi ya Dunia, kwa kuwa mwanariadha wa kwanza mwenye umri mkubwa kushinda mbio za chini ya mita 5000 katika mashindano yake ya Olimpiki mwaka 2000, alikua katika hali mbaya kutokana na kiharusi.

Mwanariadha huyo alijiandikia historia ya kuwa mkiambiaji wa kwanza kushinda mbio za mita 200 na 400 katika Olimipiki mwaka 1996 mjini Atlanta, Marekani.

Aliweza kutetea ubingwa wake katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2000 mjini Sydney, Australia wakati huo akiwa na miaka 33 na siku 12 na kuwa mwanariadha wa kwanza mwenye umri mkubwa kutwaa mataji hayo.

Hata hivyo jana alisema kupitia mitandao ya kijamii kuwa anaendelea vizuri kidogo ingawa bado yupo kitandani, akipambana na ugonjwa huo uliompata wiki iliyopita.

Aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa angalau kwa sasa anajisikia ahueni ukilinganisha na mwanzo ambapo alikuwa hawezi hata kuchezesha mkono wake achilia mbali kunyanyuka kitandani.

“Nawashukuru madaktari wamefanya kazi kubwa, hivi sasa nina nafuu kidogo ingawa bado nipo kitandani baada ya kupatwa na kiharusi,” alisema.

Advertisement