Kiiza aipa Simba Ubingwa

Muktasari:

  • Mganda huyo ametoa asilimia 80 kwa Simba kuchukua ubingwa msimu huu.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa Simba Mganda Hamis Kiiza amesema Wekundu wa Msimbazi watatwaa ubingwa Ligi Kuu msimu huu.

Simba inaongoza na pointi 58, akifuatiwa na Yanga yenye pointi 47, Azam FC (46),  Tanzania Prisons (37) na Singida United (36).

Kiiza anayecheza Al-Hilal ya Sudan alisema Simba inauwezo wa kutwaa ubingwa kwa asilimia 80, kwa sababu kuna kila dalili ya kikosi hicho kinachofundishwa na Mfaransa Pierre Lechantre kuutwaa na hizo 20 zilizobaki ndiyo zitakwenda kwa timu hizo nyingine ikiwemo Yanga.

"Simba ina nafasi ya kutwaa ubingwa kwani wapo kwenye morali wa hali ya juu, wapambana kuhakikisha  wanafanikiwa kupata matokeo, lakini kitu kikubwa tu ni kwamba wasibweteka kutokana na kuongoza na wawaangalie wanaowafuata nyuma yao," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.

AIZUNGUMZIA APRILI 29

Kiiza amekwenda mbali na kuuzungumzia mchezo wa Simba na Yanga ambao utachezwa Aprili 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa timu itakayojiandaa vizuri na kuonyesha nidhamu ya mchezo ndiyo atakayefanikiwa kushinda mechi hiyo.

"Ubingwa ni kitu kingine na kushinda mechi ya watani pia ni kitu kingine, kwani timu hizo zinapokutana hazijawahi kuisha kuonyesha ushindani kila mmoja akitaka mashabiki wake wafurahi," alisema Kiiza.