Washindi Kili Marathon kushindana Sauzi

Muktasari:

Wanariadha wanne wa Tanzania wanawake wawili na wanaume wawili kushiriki Sanlam Cape 

Dar es Salaam. Wanariadha wanne wa Tanzania watakaofanya vizuri katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon 2018 watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya jijini Cape Town baadaye mwaka huu.

Mwandaaji wa mashindano hayo, John Addison alisema lengo la mpango huo ni kuwatia moyo wanariadha wa Tanzania na kuongeza ushindani kwenye mashindano ya mwaka huu.

“Tutawapa nafasi wanariadha Watanzania kushiriki mashindano ya ‘Sanlam Cape Town Marathon’. Haya ndio mashindano pekee ya marathon barani Afrika yanayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).

“Mashindano haya huendeshwa kila mwaka kwa ushirikiano kati ya WPA, Jiji la Cape Town na taasisi inayofahamika kama ASEM Running yenye majina ya wanariadha wakubwa nchini humo, Elana Meyer na Francois Pienaar,” alisema Addison ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utalii ya Wild Frontiers.

Alisema ofa hiyo ni kwa ajili ya Watanzania pekee watakaofanikiwa kukimbia na kukaribia walau viwango vilivyopangwa na waandaaji wa Kilimanjaro Marathon 2018; Watanzania wanne watakaomaliza mashindano.

Muda uliowekwa kwa marathoni kwa wanaume ni saa 2:18 na wanawake ni saa 2:42, huku kwa upande wa nusu marathon wanaume ni saa 1: 5, wakati wanawake ni saa 1:17. Kila kundi litatoa mwanamke mmoja na mwanaume mmoja.

Addison alisema udhamini huo utahusu gharama zote kwa wanariadha wanne kwa siku tano jijini Cape Town, ada ya ushiriki na usafiri wa ndani.

“Pia tutawagharamia viongozi wawili kwenye tukio hilo. Kwa sasa tunatafuta kampuni ya ndege itakayodhamini tiketi,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha riadha nchini, Wilhelm Gidabuday aliwasifu waandaji wa Kilimanjaro Marathon kwa juhudi zao za kuinua michezo hasa riadha nchini.

“Udhamini huu wa kwenda Afrika Kusini utawapa nafasi wanariadha wa Tanzania kujitathimini na kupambana na wenzao walio katika ubora wa juu zaidi. Tunatumaini kwamba watafanya vizuri,” alisema Gidabuday.

Mashindano ya kimataifa ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2019 yanatarajiwa kuwashirikisha wakimbiaji bora kutoka Afrika Kusini.

Mbio za mwaka huu za Kilimanjaro Marathon zinazotarajia kufanyika Jumapili ya Machi 4, mjini Moshi, ambapo zaidi ya wanariadha 10,000 wanatazamiwa kushiriki chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager (42km), Tigo (21km) na Grand Malt (5km).

Wadhamini wengine ni First National Bank, Kilimanjaro Water, Diamond Motors Ltd, Kibo Palace, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Simba Cement, KNAUF Gypsum, AAR wanaojishughulisha na afya katika mashindano hayo.

Mbio hizi huandaliwa na WildFrontiers na Deep Blue Media na kuratibiwa na Executive Solutions ambayo ni kampuni ya Kitanzania.