Kilichoiponza Stars hiki hapa

Muktasari:

  • Kukosa umakini kwa safu ya ulinzi ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, kumetajwa ndiyo sababu kubwa iliyochangia kufungwa bao 1-0 na Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani Cameroon.

Maseru/Dar. Uzembe wa safu ya ulinzi uliofanywa na mabeki wa timu ya  Taifa, ‘Taifa Stars’ umeiweka katika mazingira magumu ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika, baada ya kuchapwa bao 1-0 na Lesotho.

Matokeo ya jana yaliwapa simanzi Watanzania ambao walikuwa na matumaini Taifa Stars ingeshinda mchezo huo. Katika maeneo mengi, idadi kubwa ya mashabiki walionekana kujawa na simanzi baada ya mpira kumalizika.

Katika maeneo mengi nchini mashabiki walikuwa wakifuatilia mchezo huo katika maeneo tofauti zikiwemo klabu za starehe, bar na mabanda ya kuangalia video.

Taifa Stars iliyoingia kipindi cha kwanza ikifahamu inahitajika kupata ushindi, ilipoteza matumaini, baada ya kuruhusu bao hilo dakika ya 71 baada ya kipa Aishi Manula kushindwa kupangua vyema mpira uliopigwa kutoka upande wa kulia.

Basia Makepe alifunga bao hilo kwa kichwa kutokana na mpira wa kona  uliowapita wachezaji watatu kabla ya kujaa wavuni wakati Manula akiwa amepotea. Taifa Stars itamaliza mchezo wake kwa kuvaana na Uganda jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Lesotho iliyokuwa ikishika mkia katika Kundi L ina pointi tano sawa na Taifa Stars. Uganda imeshafuzu kwa pointi 13 baada ya juzi kuilaza Cape Verde bao 1-0. Cape Verde ina pointi nne.

Salama ya Taifa Stars kufuzu fainali hizo ni kuifunga Uganda ‘The Cranes’ na kuomba dua timu za Cape Verde na Lesotho zitoke sare ya aina yoyote katika mechi zao za mwisho.

 

Mchezo wenyewe

Taifa Stars ilitengeneza nafasi dakika ya 18 baada ya kupata pasi ya mgongeo kutoka kwa Abdallah Kheri na mpira kumfukia Shabani Chilunda aliyepiga shuti lililodakwa na kipa wa Lesotho.

Dakika 20 Kheri alifanya makosa kurudisha mpira mfupi Manula ambao nusura ulete madhara kabla ya mabeki kuokoa baada ya mpira kugonga mwamba wa pembeni.

Pengo la Samatta lilionekana kuitesa Taifa Stars, baada ya nafasi nyingi kupotezwa na kukosa umakini kwa washambuliaji Saimon Msuva na Chilunda.

Wenyeji walitumia zaidi mawinga wenye kasi kuanzisha mashambulizi jambo lililoiweka safu ya ulinzi ya Taifa Stars kuwa macho wakati wote.

Mara kwa mara Manula na mabeki wake walifanya kazi ya ziada kuokoa mashambulizi ya washambuliaji Nkau Lerotholi na Tsepo Tolorane ambao walikosa mabao.

 

Kauli za wadau

Matokeo hayo (sare au kufungwa) yamewaibua nyota wa zamani wa Taifa Stars waliocheza Fainali za Afrika (Afcon) mwaka 1980, Peter Tino, Mohamed ‘Adolf’ Rishard na Juma Pondamali, ambao kwa nyakati tofauti wakizungumza na gazeti hili walisema bado timu hiyo ina nafasi ya kusonga mbele.

"Enzi zetu tunatafuta tiketi ya kucheza Afcon, timu iliyokuwa inakwenda kwenye kila kundi ilikuwa moja, sasa timu mbili," alisema Rishard aliyekuwa mmoja wa nyota wa kikosi hicho katika miaka ya 1980.

"Tumebaki na nafasi moja ambayo iko wazi kwa timu zote tatu kufuzu, kifupi mechi ya mwisho kwenye kundi hili ni ngumu, naweza kuifananisha na vita cha msingi wachezaji wanatakiwa kutulia,” alisema Rishard.

Peter Tino alisema mechi ya jana ilikuwa ya Taifa Stars kuweka historia ambayo haijawekwa kwa miaka 38 tangu ilipocheza fainali hizo mwaka 1980.

"Ilikuwa lazima tushinde, matokeo ya sare, au kufungwa hayakuwa na tija kwetu, lakini hatuna namna tunapaswa kupambana, tumejiwekea mazingira magumu wenyewe, hivyo mechi ya mwisho, lazima tufie uwanjani," alisema Tino aliyefunga bao lililoipa nafasi Taifa Stars kufuzu  Afcon mwaka 1980.

Kipa aliyeiongoza Taifa Stars katika fainali za mwaka 1980, Pondamali alisema kwa matokeo iliyopata timu hiyo ni wazi kwamba mechi za mwisho za kundi hilo siyo za masihara.

"Tuliumia sana wakati wa Maximo (Marcio aliyekuwa Kocha wa Stars kutoka Brazil) tulipokosa nafasi, kama tukipoteza na hii, huwezi kujua miaka ijayo kama tutafika wachezaji wanapaswa kutambua bendera ya Taifa wameibeba wao," alisema Pondamali.

 

Safari ya Taifa Stars

Taifa Stars ikiwa chini ya kocha mzawa Salum Mayanga ilianza safari ya kwenda Cameroon kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho mchezo uliochezeshwa na mwamuzi Djamal Aden kutoka Djibouti, jijini Dar es Salaam.

Septemba 8, upepo wa sare uliendelea kwa Taifa Stars baada ya kutoka suluhu na Uganda ‘The Cranes’ kwenye Uwanja wa Taifa wa Mandela, timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Mnigeria Emmanuel Amunike.

Katika mchezo wa tatu, Taifa Stars ilikwaa kisiki baada ya kuchapwa mabao 3-0 ugenini ilipovaana na Cape Verde  Oktoba 12 kwenye Uwanja wa wa Taifa wa Cape Verde kule Praia.

Siku nne baada ya mechi hiyo, Taifa Stars ilifufua matumaini ya kufuzu baada ya kulipa kisasi kwa Cape Verde ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo ulimvutia Rais John Magufuli ambaye aliialika Taifa Stars Ikulu, Dar es Salaam ambapo pamoja na kula chakula na wachezaji, aliipa Sh50 milioni za maandalizi ya mechi dhidi ya Lesotho.

Taifa Stars itahitimisha mechi zake za kufuzu fainali hizo Machi 22 dhidi ya Uganda ambayo tayari imeshafuzu ikiwa na pointi 10, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Lesotho ikifunga dimba na Cape Verde ambayo ilinyolewa bao 1-0 na Uganda juzi.

 

Mabao ya Taifa Stars

Ukiachana na mafanikio ya timu kwa ujumla, kwenye matokeo ya mechi nne ukiondoa ya jana, Taifa Stars imetoka sare mara mbili, imefungwa mara moja na kushinda moja.

Mabao yake matatu yaliyoipa nafasi Taifa Stars yalifungwa na nyota wa kimataifa, Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Samatta alifungulia pazia la mabao Taifa Stars dakika ya 28 dhidi ya Lesotho jijini Dar es Salaam.

Nyota huyo aliifungia Taifa Stars ilipata bao dakika ya 57 katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde huku akitoa pasi ya bao lililofungwa na Msuva dakika ya 29.

Timu zilizofuzu Afcon

Kabla ya mechi za jana, timu tisa zilikuwa zimefuzu ambazo Cameroon, Madagascar, Tunisia, Misri, Senegal, Uganda, Nigeria, Mali na Morocco.

 

Stars Afcon 1980

Taifa Stars wakati huo ikiwa chini ya Kocha Slowmir raia wa Poland akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama ilifuzu fainali hizo zilizofanyika Lagos, Nigeria.

Agosti 26, 1979 Taifa Stars ilicheza na Zambia mchezo wa marudiano uliochezwa katika mji wa Ndola, Zambia. Timu hiyo ilihitaji sare ya yoyote kufuzu fainali hizo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam lililofungwa na Rishard.

Katika mchezo wa marudiano, Taifa Stars ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 hadi dakika ya 85 ilipopata bao la kusawazisha lililofungwa na Tino.

Kikosi cha Taifa Stars katika mchezo huo kilikuwa hivi; Juma Pondamali, Leopard ‘Tasso’ Mukebezi, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omar Hussein, Peter Tino, Mohammed Salim na Thuweni Ally.

Fainali za Nigeria

Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na Nigeria, katika mchezo wa ufunguzi, ilitoka sare 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa 2-1 dhidi ya Misri na kutolewa katika hatua ya makundi.