Kipa namba moja Kenya aitaka Yanga

Muktasari:

  • Farouk Shikalo aling’ara katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Afrika

Dar es Salaam. Kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Kenya, ‘Harambee Stars’, Farouk Shikalo, amesema ndoto yake ni kucheza kwa mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga.

Shikalo ndiye alikuwa kipa namba moja wa Harambee Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019).

Akizungumza na gazeti hili jana, Shikalo alisema yuko tayari kujiunga na Yanga kwa kuwa ni klabu kubwa Afrika.

Kauli ya Shikalo anayecheza Bandari ya Kenya, imekuja siku chache baada ya kipa namba moja wa Yanga Benno Kakolanya kuigomea klabu hiyo kutokana na matatizo binafsi na uongozi.

Kipa huyo alisema ana taarifa viongozi wa Yanga na Bandari wapo katika mazungumzo kuhusu usajili wake wa dirisha dogo kabla ya kufungwa Jumamosi wiki hii.

Shikalo alisema anaona fahari kuwemo katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa na Yanga yenye historia ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 27.

Kipa huyo mwenye miaka 23, alisema ana matumaini baada ya kujiunga na Yanga milango yake itafunguka katika soka la kimataifa.

“Nimeambiwa Yanga wamepiga simu kwa uongozi wetu, kuulizia upatikanaji wangu. Ni taarifa ambazo nimezifurahia kuona timu kubwa kama hiyo imeona nina kitu cha kuongeza katika klabu yao.

“Utayari wangu wa kucheza Yanga upo kwasababu ni timu kubwa Afrika Mashariki, nikijiunga nayo nitashinda mataji, pia nitapata nafasi ya kuonyesha uwezo wangu kimataifa,”alisema Shikalo.

Pia mchezaji huyo alimtaja kocha wa zamani wa makipa Yanga Mkenya Razack Siwa ndiye kiungo wa mpango wake wa kujiunga na Yanga.

Shikalo alisema anatambua Ligi Kuu ni ngumu kwa kuwa amekuwa akiifuatilia kwa karibu kupitia mchezaji Abdallah Hamisi, Mtanzania anacheza naye Bandari.

Akizunguma jana, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema amekabidhi ripoti yake ya ufundi kuhusu usajili wake kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga, hivyo hawezi kuzungumzia ujio wa Shikalo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema hawana mpango wa kuongeza kipa mpya kwa kuwa Yanga ina makipa watatu Benno Kakolanya, Ramadhani Kabwili na Nkizi Kindoki.

Mtendaji Mkuu wa Bandari, Edward Odour alisema wamepokea maombi ya Yanga kuhusu hitaji la kipa huyo, lakini hawawezi kumpiga bei kwa kuwa ni kipa namba moja wa kikosi hicho.

“Ni kweli maombi hayo yapo, lakini hatuwezi kumuachia tuna malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, tungependa kubaki na wachezaji wenye viwango vya juu kama Farouk ni ngumu kumuachia,”alisema Odour.

Shikalo alitwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita akiwapiku Patrick Matasi aliyekuwa Tusker kabla ya kujiunga na St George’s ya Ethiopia na Kevin Omondi wa Sony Sugar. Msimu uliopita 2017/2018 aling’ara Bandari na kuipa nafasi ya pili akicheza mechi 33.

Kabla ya kipa huyo kujiunga na Bandari mwaka jana, aliwahi kucheza klabu mbalimbali nchini Kenya zikiwemo Muhoroni FC, Posta Rangers FC, Tusker FC na FC Talanta.