VIDEO: Kisa hujuma: Mashabiki Simba wamtimua kiongozi

Muktasari:

  • Simba imekuwa ikipata ushindani mkali kila inapocheza na Mbao katika jiji la Mwanza

Mwanza. Mashabiki wa Simba wamezua taharuki katika Hotel ya Lenana Jijini Mwanza ilipofikia timu yao kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao unaotarajiwa kupigwa kesho Alhamisi kwenye Uwanja la CCM Kirumba.

Mabingwa hao watetezi wametua leo asubuhi Jumanne kwa ndege ya Air Tanzania na kupokelewa kwa shangwe kali na mashabiki wakiwa katika magari na pikipiki na kuisindikiza timu yao kutoka uwanja wa Ndege hadi Hotel waliyofikia.

Ghafla baada ya wachezaji kuingia ndani kwa ajili ya kunywa chai, nje ya hotel hali ilibadilika huku sauti za vuvuzera zikianza kurindima na nyimbo zikaanza kuimbwa za kumfukuza Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Mwanza, Omary Makoye kwa madai ya kuihujumu timu yao.

Hata hivyo baadhi ya viongozi walioambatana na timu walipotoka nje kujaribu kuwatuliza mashabiki hao, hawakuwa tayari kuwasikiliza viongozi hao na msimamo ukabaki palepale kumtaka kiongozi huyo atolewe nje.

Purukushani iliendelea kwa mashabiki na viongozi hao wakibishana kwa kitendo hicho, baadaye Mwenyekiti huyo alichomoka ndani kimya kimya na kutokomoea kusikojulikana.

Madai ya mashabiki hao yalikuwa kuwa kiongozi huyo anahusika katika njama za kuihujuma Simba pindi inapokuja kucheza katika mikoa ya Kanda ya Ziwa haswa Mbao na kusababisha kupata matokeo kwa taabu.

Mmoja wa mashabiki Juma Nassoro alisema kuwa mbali na kuihujumu Simba, lakini kiongozi huyo amekuwa akichukua pesa za mashabiki akiwadanganya kufanya shughuli za timu, lakini imekuwa tofauti.

“Aondoke kabisa hatumtaki mtu kama huyu anayeshiriki kuihujumu timu na kuchukua michango haijulikana inafanya nini, Simba ni timu kubwa,”alisema Nassoro.

MCL Digital ilimshuhudia kiongozi huyo akiondoka kimya kimya hadi kujihifadhi kwenye kituo cha Afya cha Acess Medical kwa ajili ya usalama wake na kumfuata kuzungumza naye juu ya tukio hilo na kuongea kwa uchache akiwa ametulia.

“Nimeshajua sababu yao hao, ila najua wametumwa tu, lakini kinachowasumbua tena wana uchu wa madaraka ila ngoja natarajia kutangaza rasmi kuijiuzuru ili waendelee wao,” alisema Makoye.

Hata hivyo baadaye hali ilitulia kwa mashabiki hao na kuanza kushangilia lazima timu yao ishinde mchezo wao dhidi ya Mbao na kwamba hawana wasiwasi na kikosi chao.