Kiungo mpya aitikisa Yanga

Muktasari:

Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo yupo kwao Mbeya na jana Jumatano kama mazungumzo hayo yangekamilika basi angesaini na kujiunga moja kwa moja na Yanga ambayo ipo jijini Mbeya.

MCHANA wa jana Jumatano, mabosi wa Yanga waliitana faragha na meneja wa kiungo Kenny Ally ili kujadili dili la kumsainisha atue Jangwani, lakini mpango ulitibuka baada ya pande mbili kushindwa kuafikiana, huku mwenyewe akifungua alivyojipanga.

Ni hivi, Yanga walipanga kumsajili Kenny kwa mkataba wa miaka miwili kwa kuli[pa fedha kwa mafungu, lakini meneja huyo akawagomea akitaka mteja wake asaini mwaka mmoja kwa dau lenye thamani ya Sh12 milioni tena bila ya mafungu.

Habari za ndani kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu wa meneja wa mchezaji huyo, Maka Mwalwisi zinasema Yanga wao wakitaka kutoa Sh20 milioni kwa miaka miwili, lakini wangelipa kwa mafungu ya awamu mbili.

Inaelezwa, kikao hicho kilifanyakia ofisi ya mmoja wa vigogo wa Yanga iliyopo Masaki na baada ya kushindikana ilielezwa kila mmoja kwenda kufikiria ili kesho Ijumaa watakapokutana wawe na jibu moja.

Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo yupo kwao Mbeya na jana Jumatano kama mazungumzo hayo yangekamilika basi angesaini na kujiunga moja kwa moja na Yanga ambayo ipo jijini Mbeya.

“Mpaka muda huu mchana hakuna maafikiano, kila upande umeomba kujifikiria ili wakutane tena keshokutwa (kesho Ijumaa), mvutano upo kwenye vipengele vya mkataba pamoja na pesa ya usajili, Yanga wanataka miaka miwili lakini mchezaji anataka mwaka mmoja.

“Lakini naamini wakitafakari kila mtu atakuwa na maamuzi sahihi ya nini kifanyike maana ni kweli Yanga wanamhitaji Kenny na kuna viongozi wapo Mbeya wanasubiri majibu ya huku ili wamsainishe kule kule na kujiunga na timu mara moja,” kiliseam chanzo.

Mwanaspoti lilimtafuta Mwalwisi aliyejibu kwa kifupi; “Bado hajuafikia makubaliano ya mwisho, kuna mambo tumepeana muda kwenda kutafakari na kuyatolea maamuzi, unajua mambo ya mikataba ni ya kisheria, hivyo lazima uyapitie kwa umakini.”

“Lolote linaweza kutokea kama ni leo (jana) jioni ama keshokutwa (Ijumaa kesho) kwani hakuna uharaka wowote muda bado upo wa usajili, ikishindikana kufikia makubaliano basi ataendelea na Singida United, tusubiri muda ufike mtajulishwa.”

KENNY ANENA

Kwa upande wa Kenny alisema hakuna mchezaji anayemhofia Yanga na kuweka wazi hata Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye amekuwa kipenzi cha klabu hiyo msimu huu.

“Nipo Mbeya nina msiba, ila mazungumzo na Yanga kuhusu mimi kuitumikia msimu huu yanaenda vizuri ila kwasasa nahangaikia tatizo hili nililonalo,” alisema.

Kenny pia alimzungumzia Raphael Daud aliyedai ni pacha wake tangu wakiwa wote City kwa wanajua namna ya kutengenezeana nafasi za kufunga, hivyo anaamini siku akipata nafasi ya kucheza tena pamoja atakuwa huru kuuchezea mpira atakavyo.