Kiwango cha Arsenal chamkuna Cech

Muktasari:

  • Cech raia wa Jamhuri ya Czech, aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa jana usiku kati ya Arsenal na Everton, alisema naona kikosi hicho cha Kocha Unai Emery, kipo kwenye kiwango bora.

London, England. Kipa wa Arsenal, Petr Cech, amesema kuwa timu hiyo imerejea kwenye kiwango bora na hivyo anaamini kuwa hivi sasa inaweza kupigania ubingwa.

Cech raia wa Jamhuri ya Czech, aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa jana usiku kati ya Arsenal na Everton, alisema naona kikosi hicho cha Kocha Unai Emery, kipo kwenye kiwango bora.

Alisema washambuliaji wapya Alexandre Lacazette na shujaa kutoka Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang, wamekuja na moto wa aina yake na ndio walioirejesha timu hiyo katika ushindani wa ligi.

“Nadhani kwa sasa timu imepata nguvu mpya ujio wa Aubameyang na Lacazette umeifanya timu iwe na uwezo wa kufunga mabao tofauti na msimu uliopita,” alisema. 

Alisema msimu uliopita Arsenal ilikuwa ikikabiliwa na ubutu wa safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inashindwa kupata mabao katika baadhi ya mechi jambo lililoiondoa kwenye mbio za ubingwa mapema.

Alisema tangu kutua Lacazette amekuwa akifunga au kusababisha bao katika kila mechi sawa na ilivyo kwa Aubameyang.

Washambuliaji hao wawili kila mmoja amefunga mabao matatu katika mechi tano zilizopita, jambo linalomfanya Cech kuamini kuwa, hivi sasa timu hiyo imerejea kwenye ushindani wa mataji.