Tuesday, November 21, 2017

Liverpool yamuonya Sturridge

 

London, England. Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp, amemtaka mshambuliaji Daniel Sturridge kuelekeza nguvu katika kikosi hicho.

Kauli ya Klopp imekuja muda mfupi baada ya kuibuka tetesi kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England anatataka kuondoka katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Kocha huyo alimwambia Sturridge kuwa anahitaji wachezaji wote Liverpool kuisaidia klabu hiyo katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund amemtaka Sturridge kuweka kando matatizo binafsi na kujikita katika maendeleo ya klabu.

Klopp alisema mkakati wa Liverpool ni kuvuna pointi za kutosha katika kipindi cha msimu wa Sikukuu ya Krismasi.

“Nahitaji wachezaji wote wawe na furaha, siwezi kumpa nafasi ya kucheza mechi nyingi mchezaji ambaye ana matatizo binafsi,” alisema Klopp.

Mchezaji huyo anadaiwa kusaka  timu mpya ambayo atapata nafasi ya kucheza ili kumshawishi kocha Gareth Southgate kumuita katika kikosi cha England kwa fainali za Kombe la Dunia.

Ingawa mshambuliaji huyo hakuitwa katika mechi mbili za kufuzu fainali hizo dhidi ya Ujerumani na Brazil, lakini ana matumaini ya kwenda Russia endapo atapata nafasi ya kucheza mechi nyingi za klabu.

Sturridge amekosa namba katika kikosi cha kwanza msimu huu na Klopp amekuwa akiwatumia Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino katika safu ya ushambuliaji.

 

 

-->