Kocha: Nkana hawachomoki

Kitwe/Dar. Simba imemaliza dakika 90 za kwanza, mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Nkana FC hapa Kitwe, Zambia.

Mabao mawili ya Nkana yalifungwa na Kelvin Kampamba na Ronald Kampamba wakati lile la Simba lilifungwa na nahodha John Bocco.
Katika mechi hiyo Simba walionekana kufanya makosa katika safu ya ulinzi haswa mabeki wa kati huku Pascal Wawa akionekana kuzidiwa na mastraika wa Nkana.
Makosa mawili ya kutokukabahadi mwisho yaliwagharimu Simba kufungwa mabao mawili ambayo yalitokana na umakini mdogo.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema mechi hiyo walizidiwa kipindi cha kwanza kwa kuwa walikuwa wanashindwa kumiliki mpira na kupoteza mara kwa mara.

Aussems alisema anawaheshimu Nkana kwa kuwa ni timu kubwa ndio maana wamefika katika hatua hiyo lakini mechi ya marudiano ndio itaamua timu itakayofuzu. Simba inahitaji ushindi wa bao 1-0 ifuzu.

Alisema: “Kupoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 2-1 si mbaya kwani tuna uwezo wa kupindua matokeo katika mechi ya marudiano.

Tunakwenda kujipanga, kama wao wametufunga kwao na sisi tunaweza kuwafunga kwetu na tukapata matokeo ya kusonga mbele.”

Kauli za wadau

Kipa mkongwe wa zamani wa Simba, Mohamed Mwameja ‘Tanzania One’ alirejea kusema mafanikio ya Simba yako mikononi mwa kipa Aishi Manula na mabeki wake kujipanga.

“Manula anapaswa kucheza na nguvu ya mpira, wapinzani watakuwa wamemsoma na huenda wakatumia mbinu ya kusaka bao kwa kupiga mashuti ya mbali ambayo Manula amekuwa akifungwa kwa staili hiyo mara kwa mara,” alisema Mwameja.

Alisema kinachotakiwa katika mchezo wa Jumamosi, Manula aanze kucheza na muvu za mipira mara tu utakapovuka katika nusu ya uwanja kuelekea golini kwake huku akihakikisha anazungumza muda wote na mabeki wake.

Alisema hana hofu na fowadi ya Simba, ina uwezo wa kupata mabao kuanzia mawili kuendelea, lakini akatoa angalizo kwa mabeki kuanzia namba moja hadi sita.

“Nkana ni timu bora, nimewaangalia wachezaji wao baadhi ni wepesi na wana kasi, hivyo kikubwa Simba wajitahidi kuidhibiti kwa kuifunga bao la mapema ambalo litawavuruga,” alisema.

Kipa huyo nyota wa zamani alisema, kocha ameona ubora na udhaifu wa Nkana hivyo, hana shaka kwamba Simba watacheza kwa kufuata maelekezo ya kocha kulingana na alivyoisoma Nkana.

Mchambuzi wa Soka, Ally Mayay alisema mbinu kubwa kwa Simba ni kumiliki mipira na kuharakisha mashambulizi katika mchezo huo wa maruadiano ambao Simba ina faida ya bao la ugenini.

“Nafasi bado ipo kwa Simba, bao moja walilolipata ugenini litengeneze mkakati wa kuwavusha hatua ya makundi, wahakikishe wanacheza ‘direct football’.

“Mpira ukitoka nyuma, upite kati na kwenda mbele, viungo wasichezee mipira muda mrefu katikati hiyo itawapa mabeki wa Nkana nafasi ya kujipanga,” alisema Mayay.

Alisema Simba inapaswa kuwafanya mabeki wa Nkana kuwa bize kwa kupeleka mashambulizi muda wote huku wakihakikisha hawaruhusu kufungwa bao lolote nyumbani ambalo litawapa faida Nkana ya bao la Ugenini.