Wednesday, January 3, 2018

Kocha Mbeya City awasha moto kupoteza pointi tatu

 

By Justa Musa

Mbeya. Kocha Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nswanzurwimo amesema hawakustahili kupata pointi moja kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar lakini kutojitambua kwa washambuliaji kumeigharimu timu hiyo.

Mchezo huo uliochezwa jana Jumanne baada ya kuahirishwa siku ya Jumatatu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa, ulishuhudiwa timu hizo zikitoshana nguvu na kugawana pointi moja moja.

Nswanzurwimo alisema mfumo alioupanga hususani kwa washambuliaji watatu haukufutwa na badala yake mshambuliaji mmoja ndiye aliyeonekana kujitambua.

“Mastraika wangu hawakusikia vizuri huu mfumo wetu ambalo tuliupanga maana tungecheza na mastraika watatu lakini wao hilo hawakulitambua na badala yake walimuachia mmjoa wa kati huku wao wakiwa pembeni kabisa,’’alisema Nswanzurwimo.

Alisema ataendelea kuyafanyia kazi makosa hayo yaliyojitokeza ili kuona jinsi gani anacheza na mastraika watatu ambao wataisaidia timu kupata matokeo mazuri kwa kila mechi.

Kocha huyo Mganda alisema shida kubwa iliyosababisha timu hiyo kupoteza mechi nne mfululizo ni wachezaji kutokuwa  na saikolojia nzuri pamoja na hali ya kujiamini kushuka  kila walipokuwa wakiingia kwenye mechi.

Hata hivyo Nsawanzurwimo alifurahi kwa timu yake kuambulia pointi hiyo moja na kwamba sasa wamepata mwanga wa kufanya vizuri hata kwa mechi zijazo.

Kwa Upande wake Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema walikuja Sokoine na mipango yao ya kuchukua pointi tatu lakini kutokana na wapinzani kujipanga zaidi kumesababisha wagawane poiti moja moja.

‘’Wenzetu hawa wametoka kupoteza mechi nne mfululizo ,kwa hiyo huu mchezo wa leo (juzi) walijipanga kuzuia zaidi na kupata matokeo ya pointi tatu kwa namna yoyote ile na hapo ndiyo ugumu wa mchezo ulipokuwepo,’’alisema Mexime.

-->