Kocha PSG asema hataidharau Man United

Muktasari:

  • Kocha wa timu ya PSG, Thomas Tuchel amesema kuwa kupangwa ni timu ya Manchester United ni mtihani mgumu kwake ambao anapaswa kufaulu, akisema atacheza nayo kwa tahadhari hataidharau kama baadhi ya mashabiki na wadau wa soka wanavyodhani kuwa timu hiyo kwa sasa imeporomoka, akisema anamjua kocha Jose Mourinho anavyotisha kwa mechi za mtoano

Paris, Ufaransa. Kocha wa timu ya Paris St Germain, Thomas Tuchel, amesema atakiandaa kikosi chake kucheza na Manchester United katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kuweka dharau.

Alisema kufanya vibaya katika baadhi ya mechi za msimu huu hakuondoi ukweli kuwa Man United ni moja ya timu kubwa barani Ulaya yenye wachezaji wazoefu na kocha mbunifu, Jose Mourinho, ambaye kwa mechi za mtoano ni mjanja sana.

Kocha huyo anatambia kiwango cha kiungo wake Angel Di Maria, pamoja na safu tishio ya ushambuliaji inayoongozwa na mkongwe Edson Cavani, Neymar, pamoja na chipukizi Kylian Mbappe.

“Nilijua katika droo ya 16 bora chochote kinaweza kutokea, tumepangiwa Man United timu yenye uzoefu wa mashindano ya Ulaya, watu wanaibeza kuwa haifanyi vizuri lakini hadi kufika hapa ni timu bora hatutafanya kosa la kuidharau,” alisema Tuchel.

Alisema kuwa wachezaji wake wanapaswa kuichukulia timu hiyo kwa umakini mkubwa hapo Februari, 2019 watakapokutana katika mchezo wa kwanza kabla ya marudiano Machi mwakani.

Kocha huyo alisema timu yake itapambana kusaka ushindi katika mechi zote mbili ya nyumbani na ugenini kwani anajua fika Man United sio timu ya kutabirika inaweza kubadili matokeo wakati wowote.

Tuchel alisema kuwa hawatakubali kufanya makosa kama waliyoyafanya walipokutana na Liverpool katika mchezo wa kwanza wa makundi ambapo walifungwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Anfield ingawa walishinda mechi ya marudiano.