Kocha tenisi Tanzania aula Shelisheli

Muktasari:

  • Leringa aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa na klabu ya Gymkhana Arusha, ameingia mkataba wa miaka miwili na Chama cha Tenisi Shelisheli (STA).

Arusha: Kocha wa mchezo wa tenisi nchini, Nicolas Leringa amepata kazi ya kuifundisha timu ya Taifa ya Shelisheli.

Leringa aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa na klabu ya Gymkhana Arusha, ameingia mkataba wa miaka miwili na Chama cha Tenisi Shelisheli (STA).

Akizungumza kwa simu jana, Leringa alisema Shelisheli walimuona baada ya kubaini uwezo wake akiwa nchini humo kwa miaka 10 alipokuwa akifundisha tenisi nchini humo.

“Nilikuwa huku miaka 10 iliyopita nilijifunza na kufundisha mchezo wa tenisi, baadaye nilirejea nchini kuendelea kufundisha zaidi vijana kuliko timu kubwa hata timu ya Taifa kwa sababu napenda watoto,” alisema Leringa.

Kocha huyo alisema Serikali inatakiwa kuwekeza katika mchezo huo kwa kuwajengea msingi mzuri wachezaji vijana ambao watakuwa hazina kwa timu za Taifa.

“Tunachokosea Chama cha Tenisi Tanzania (TTA) hakina mkakati na miongozo endelevu ya mchezo huu, hivyo hata ukiwa na walimu na wachezaji wenye vipaji ni vigumu kufikia malengo mtakayoweka watu wachache,” alisema Leringa.

Kocha huyo alisifika kwa kuibua vipaji vya wachezaji chipukizi akiwa Gymkhana Arusha na miongoni mwa nyota wanaotamba katika mchezo wa tenisi ni Goodluck Mollel, Johnson Shayo, Frank Benard na Omari Sulle.