Mwakyembe ataka ubingwa kuogelea Afrika|2

Muktasari:

  • Tanzania katika mashindano hayo inashindana na timu za kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, na Sudan

Dar es Salaam. Waziri wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka timu ya Taifa ya kuogelea kupambana na kubakisha kombe la ubingwa wa Afrika linabaki nchini.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 19 wakati akifungua mashindano ya Afrika ya Cana ya kanda ya tatu yanayoendelea kwenye bwawa la kuogelea la Hopac jijini Dar es Salaam na kushirikisha nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Sudan na wenyeji Tanzania.

"Nimeambiwa nyinyi (Timu ya Tanzania) ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo, naamini rekodi yenu itabaki pale pale msimu huu," alisema Mwakyembe ambaye pia aliahidi kusimamia mchakato wa ujenzi wa mabwawa ya kuogelea hapa nchini.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha kuogelea Tanzania (TSA), Phillip Saliboko alisema Tanzania inawakilishwa na timu mbili, Tanzanite ambayo itakuwa na jumla ya wachezaji 30 na ya pili inajulikana kwa jina la Platinum itakuwa  na wachezaji 21.

“Maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wamepata maandalizi Timu hizo zipo kambini hotel ya Giraffe chini ya makocha, Alexander Mwaipasi na Michel Livingstone, tuna matumaini makubwa ya kufanya vyema,” alisema Saliboko.

Mmoja wa makocha wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi alisema kuwa wamemaliza mafunzo yao yote kwa waogeleaji hao na wanatarajia kupata ushindi mkubwa.

“Kazi ya kufundisha tumemaliza, iliyobaki sasa ni waogeleaji kufanya mambo yao kwenye bwawa, lengo ni kutetea ubingwa, tupo tayari kwa mashindano,” alisema Mwaipasi.

Alisema kuwa timu yao inaundwa na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na wanaamini wataonyesha uwezo wao na thamani yao ya kuwa katika timu ya Taifa.

“Nawapongeza sana wadhamini, Giraffe Hotel,  Vodacom Tanzania, Swissair, JCDecaux,  Coca Cola, Label Promotions , Print Galore na Slipway Hotel. Wametuwezesha kufanya maandalizi makubwa katika mashindano haya, hatuta waaangusha,” alisema.

Mbali ya Tanzania, mashindano hayo pia yatashirikisha waogeleaji kutoka nchi za Uganda, Zambia, Afrika Kusini,  Sudan, Kenya na wenyeji Tanzania ambayo itawakilishwa na timu mbili.

Wachezaji wanaoumda timu ya Tanzanite ni Rania Karume , Chichi Zengeni, Maia Tumiotto, Smriti Gokarn, Sonia Tumiotto, Anjani Taylor ambao wote wanatoka klabu ya DSC, huku wengine ni Natalie Abwooli Sanford (MIS), Anna Guild, Emma Imhoff (MSC), Sanne Kleinveld ( ISM Moshi),  Angelica Spence, Tara Behnsen, Tami Triller,Kayla Gouws na Amani Doggart ambao wanatoka klabu ya Taliss.

  Wachezaji wanaume ni Judah Miller, Elia Imhoff, Delvin Barick, Caleb O'Sullivan, Khaleed Ladha na Matthew Guild wanatoka klabu ya Mwanza, Chris Fitzpatrick (ISM Moshi), Marin DE Villard (DSC), Adil Bharmal, Hilal Hilal, Harry McIntosh, Dhashrrad Magesvaran (Taliss) na wanaotoka klabu ya shule ya kimataifa ya Morogoro ni   Joseph Sumari, Collins Saliboko na Dennis Mhini.

Wachezaji wanaounda klabu ya Platinum kwa upande wa wanawake ni  Shivan Bhatt, Natalia (Taliss), Charlotte Sanford,  Vanessa Dickson (MIS), Rebecca Guild, Meredith Boo (MSC), Maria Bachmann ( ISM Moshi), Kayla Temba na Maya Somaiya  ambao wote wanatoka klabu ya DSC.

Wanaounda timu ya wanaume ni Aravind Raghavendran, Mohameduwais Abdullatif (Bluefins), Abraham Kayugwa( ISM Moshi), Terry Tarimo,  Aliasgar Chakera(Taliss), Zeke Boos (MSC), Yuki Omari, Augustino Lucas (Champion Rise), Fallih Ahmed (Taliss), Carter Helsby (MSC), Ian Lukaza(ISM) na Emmanuel Stenson wa shule ya kimataifa ya Morogoro.